'
Thursday, February 14, 2013
CHEZEA TEGETE WEWE
MSHAMBULIAJI Jerry Tegete jana aliendelea kudhihirisha makali yake katika kutikisa nyavu za timu pinzani baada ya kuifungua Yanga mabao mawili kati ya manne katika mechi dhidi ya African Lyon.
Katika mechi hiyo ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliichapa Lyon mabao 4-0 na kuzidi kujikita kileleni mwa ligi hiyo.
Ushindi huo umeiwezesha Yanga kuendelea kuongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 16, ikiwa mbele ya Azam kwa tofauti ya pointi tatu. Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 28.
Tegete aliifungia Yanga la kwanza dakika ya 21, alipounganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa David Luhende. Aliongezea bao la pili dakika ya 42 kwa kisigino baada ya kupokea pasi kutoka kwa Simon Msuva.
Yanga ilipata nafasi nyingine nzuri za kufunga mabao dakika ya sita, 13, 24 na 35, lakini zilipotezwa na Hamisi Kiiza, Tegete na Haruna Niyonzima. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Katika kipindi cha pili, Yanga ilifanikiwa kupata penalti mbili. Ya kwanza ilipatikana dakika ya 48 baada ya beki mmoja wa Lyon kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, lakini ilipotezwa na Hamisi Kiiza baada ya shuti lake kudakwa na kipa Abdul Seif.
Penalti ya pili ilipatikana dakika ya 77 na kupachikwa wavuni na Didier Kavumbagu baada ya mchezaji mwingine wa Lyon kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Bao la nne la Yanga lilifungwa na Nizar Khalfan dakika ya 81 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Saidi Bahanuzi.
Lyon ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 50 wakati Kyata alipopewa pasi safi na Mohamed Samatta akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake lilipanguliwa na kipa Ally Mustafa wa Yanga.
Yanga: Ally Barthez, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Athumani Iddi, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Frank Domayo, Jerry Tegete, Hamizi Kiiza/Didier Kavumbagu, Haruna Niyonzima.
Lyon:Abdul Seif, Yusuf Mlipili, Sunday Bakari, Ibrahim Job, Obina Salamusasa, Abdulehan Gulam,Amani Kyata, Mohamed Samatta, Iddi Mbaga/Yusuf Mgwao, Bright Ike, Adam Kingwande.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment