MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amesisitiza uwepo umakini katika uamuzi na masuala mengine muhimu kwa nia ya kupata timu bingwa halali wa ligi kuu ya msimu huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hoteli ya JB Belmont, Dar es Salaam jana, Manji alisema kuwepo umakini katika uchezeshaji kutasaidia kupatikana bingwa halali.
Kauli hiyo ya Manji huenda imetokana na kuwepo ushindani mkali katika ligi kuu ya msimu huu, ambapo mpaka sasa Yanga inaongoza ikiwa na pointi 33, ikifuatiwa na Azam yenye alama 30 na mabingwa watetezi Simba wenye pointi 27.
Mzunguko wa pili ambao ni lalasalama, umekuwa na ushindani usio wa kawaida baada ya timu hizo tatu za juu kupiga kambi nje ya nchi kujiandaa na mtanange huo.
Yanga ilikwenda Uturuki, Simba Oman na Azam ilisafiri Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Kenya.
Katika hatua nyingine Manji, ameahidi bodi itazisaidia klabu zote za ligi kuu bila ya upendeleo licha ya yeye kuwa mwenyekiti wa Yanga.
Alisema kuwa ameomba wadhifa huo kwa nia ya kustawisha klabu zote.
Alisema klabu za ligi kuu zinahitaji kusaidiwa kwa hali na mali kwa dhamira ya kuziboresha ili zitoe upinzani unaostahili.
Manji alisema anagombea wadhifa huo kwa lengo la kuzisaidia kupata udhamini klabu za ligi kuu na kuipiga jeki kwa hali na mali timu yoyote itakayofuzu kwenye michuano ya kimataifa.
"Tunataka zote ziwe zinafaidika bila ya upendeleo na klabu yoyote ikifuzu katika mashindano ya kimataifa, itaisaidiwa pasipo kutazama ukubwa wa timu," alisema Manji.
Alisema kujitokeza wadhamini wengi katika klabu hizo kutasaidia kila moja kuwa na kipato kikubwa na kuondokana na dhana iliyojengeka sasa ya timu zenye uwezo kuwa Simba, Yanga, Azam na Mtibwa Sugar.
No comments:
Post a Comment