KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

WAERITREA WAPEWA UKIMBIZA UGANDA



KAMPALA, Uganda

SERIKALI ya Uganda imekubali kuwapa hifadhi ya ukimbizi wachezaji 15 wa timu ya soka ya taifa ya Eritrea waliozamia nchini humo.

Wachezaji hao pamoja na daktari wa timu hiyo, walitoroka kwenye kambi ya Eritrea wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika Desemba mwaka jana mjini Kampala.

Kamishna wa Wakimbizi katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uganda, Apollo Kazungu aliieleza BBC juzi kuwa, wameamua kuwapa hifadhi ya ukimbizi wachezaji hao kutokana na madai yao kukidhi maombi yao.

Eritrea ilitolewa katika hatua ya awali ya michuano hiyo baada ya kutoka suluhu na Zanzibar, kuchapwa 3-2 na Malawi na kufungwa 2-0 na Rwanda.

Baada ya kutolewa katika michuano hiyo, wachezaji 17 wa Eritrea waliondoka kwenye hoteli ya Sky ya mjini Kampala, ambako walipangiwa kukaa na kuaga kwamba wanakwenda kutembea mjini.

Hata hivyo, wachezaji hao walitokomea kusikojulikana wakati wengine watatu waliokuwa wamebaki hotelini, walirejea kwao.

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), Patrick Ogwel alisema wamefurahishwa na uamuzi huo wa serikali wa kuwapa hifadhi ya ukimbizi wachezaji hao.

"Hizi ni habari nzuri kama mamlaka zinazohusika zimeweza kulitatua tatizo hilo. Lakini siku zijazo, timu zinapaswa kuja kucheza soka na kurejea katika nchi zao,"alisema.

Kazungu alisema wachezaji wengine wawili waliokuwa wameomba hifadhi ya ukimbizi, waliamua kurejea kwao wakati wengine waliobaki waligoma kuondoka kwa hofu ya kupewa adhabu za kijeshi.

Kwa mujibu wa sheria za Uganda, raia wa kigeni wanaopewa hifadhi ya ukimbizi, hawalazimishwi kuishi kwenye kambi maalumu, badala yake wanaruhusiwa kuishi mahali popote iwapo watakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Hii ni mara ya pili kwa wachezaji wa Eritrea kuzamia katika nchi zinazounda Baraza la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) wakati wa michuano ya Chalenji na Kombe la Kagame.

Katika michuano ya 2010 iliyofanyika Tanzania, wachezaji 13 wa Eritrea walitoroka kambini na kuomba hifadhi ya ukimbizi. Baadhi ya wachezaji hao kwa sasa wako Marekani ambako wamepatiwa hifadhi.

No comments:

Post a Comment