KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 3, 2013

WANYARWANDA KUZICHEZESHA STARS NA CAMEROON



WAAMUZI kutoka Rwanda wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), wamepangwa kuchezesha pambano la kirafiki kati ya Tanzania na Cameroon litakalochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mwamuzi wa kati atakuwa Munyemana Hudu, akisaidiwa na Simba Honore na Ndagizimana Theogine. Mwamuzi wa akiba atakuwa Oden Mbaga wa Tanzania.

Wambura alisema Hudu na wenzake wanatarajiwa kuwasili nchini kesho saa 12.40 jioni kwa ndege ya RwandaAir na wamepangiwa kufikia kwenye hoteli ya JB Belmont.

Pambano kati ya Taifa Stars na Cameroon, ambalo lipo kwenye kalenda ya FIFA, limepangwa kuanza saa 11 jioni.

Wakati huo huo, kundi la kwanza la timu ya Cameroon lenye watu 13 lilitarajiwa kuwasili nchini jana saa 4.40 usiku.

Wambura alisema jana kuwa, kundi la pili linaloongozwa na nahodha wa timu hiyo, Samuel Eto’o linatarajiwa kutua leo saa 3.45 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Wambura, Eto’o anayechezea timu ya Anzhi Makhachkala ya Russia, atatua kwa ndege ya Kenya Airways akiwa na Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik.

Wambura alisema Kocha wa timu hiyo, Jean Paul Akono na msaidizi wake, Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Afrika Kusini.

Alisema kundi lingine la timu hiyo litatua 4.40 usiku kwa ndege ya KLM. Alisema kundi hilo litakuwa na beki, Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa.

Wachezaji waliobaki wakiongozwa na kiungo wa Barcelona, Alexandre Song, watawasili kesho kwa muda tofauti kwa ndege za KLM na Kenya Airways.

No comments:

Post a Comment