KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, February 7, 2015

NYOSO, MORRIS WAPEWA ADHABU KALI


 Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
 imewafungia kati ya mechi tatu na nane wachezaji Juma Nyoso wa Mbeya City
 na Aggrey Morris wa Azam kutokana na makosa ya kinidhamu waliyoyafanya
 wakiwa uwanjani.

Nyoso ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumfanyia vitendo vya udhalilishaji
 mshambuliaji Elias Maguri wa Simba amefungiwa mechi nane za Ligi Kuu ya
 Vodacom (VPL). Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 57 na Ibara ya
 11 (f) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.

 Akiwa mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 5 mwaka huu) jijini Dar es
 Salaam, Nyoso alikiri kufanya na kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi
 mchezaji Maguri kwa kitendo hicho.

Akisoma uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa
 alisema kitendo kilichofanywa na Nyoso ni kosa kubwa, kudhalilisha utu wa
 mtu, na ni mfano mbaya kwa watoto na jamii nzima ya mpira wa miguu.



 Naye Morris amefungiwa mechi tatu za VPL baada ya kutiwa hatiani kwa
 kumpiga mshambuliaji Emmanuel Okwi wakati timu hizo zilipopambana kwenye
 mechi ya ligi iliyochezwa Januari 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
 Salaam.



 Kabla ya kusoma uamuzi, Wakili Msemwa alisema mlalamikiwa Morris alikiri
 kugongana na Okwi, kwa maelezo kuwa aliingia kwenye 'reli' ndiyo ukatokea
 mgongano huo.

Kamati baada ya kupitia malalamiko ya klabu ya Simba, ripoti za Brain CT
 scan kutoka Besta Diagnostic Centre na nyingine kutoka Taasisi ya Mifupa
 Muhimbili (MOI), taarifa za madaktari zilionyesha Okwi aligongwa kichwani
 akiwa anacheza mpira na kuzimia kwa dakika tano, pia mkanda wa video
 uliowasilishwa na TFF imeona kulikuwa na kugongana kati ya wachezaji hao.

 Hivyo, Kamati ikamtia hatiani Morris kwa kutumia Ibara ya 48(1)(d) ya
 Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012 kwa kumfungia mechi hizo tatu na
 kumpa onyo kali.

 Pia Kamati hiyo imemfungia miezi sita na kumpiga faini ya sh. 200,000
 Meneja Vifaa (Kit Manager) wa timu ya Polisi Mara, Clement Kajeri kwa
 kuhamamisha vurugu na kuwapiga waamuzi kwenye mechi dhidi ya Mwadui
 iliyochezwa Uwanja wa Karume mjini Musoma. Adhabu hiyo imetolewa kwa
 kuzingatia kanuni ya 40(2) ya Ligi Daraja la Kwanza.

 Wachezaji watatu wa Friends Rangers; Mahmoud Othman, Khalid Twahil na John
 Alexander wamefungia miezi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa
 kumpiga mwamuzi kwenye mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Majimaji.

 Licha ya wachezaji hao kuitikia mwito wa Kamati, wachezaji hao walizuiwa na
 viongozi wa kuingia ukumbini wakati malalamiko dhidi yao yalipoanza
 kusikilizwa. Hatua hiyo iliifanya Kamati ifanye uamuzi baada ya kuusikiliza
 upande wa walalamikaji pekee.

 Shauri dhidi ya mchezaji George Michael wa Ruvu Shooting kwa kumchezea
 ubabe Amisi Tambwe wa Yanga, Kamati imeliahirisha baada ya mlalamikiwa
 kupata udhuru uliosababisha asiwepo.

 Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza malalamiko ya timu ya Friends Rangers
 kupinga refa kuchezesha mechi yao dhidi ya Majimaji kwenye mvua kubwa,
 kutoa maamuzi yasiyo halali na kutokuwepo na ukweli kwenye ripoti ya
 Kamishna yakasikilizwe na Bodi ya Ligi kwa vile si masuala ya kinidhamu.

No comments:

Post a Comment