KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, February 22, 2015

BEKI NGULI WA ZAMANI WA SIMBA CHRISTOPHER ALEX AFARIKI DUNIA


BEKI wa zamani wa klabu ya Simba na timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Christopher Alex amefariki dunia.

Habari kutoka mkoani Dodoma zimeeleza kuwa, Alex amefariki dunia leo baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa kifua.

Wakati huo huo, Chama cha Kandanda mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimeeleza kusikitishwa kwake na kifo cha mchezaji kiungo wa zamani wa klabu ya Simba na Taifa Stars,Christopher Alex,  maarufu kama Masawe, kilichotokea leo (Februari 22), katika Hospitali ya Mirembe, Dodoma.

Mwenyekiti wa DRFA,Almas Kasongo,amemuelezea marehemu Christopher kuwa ni mchezaji aliyevuma enzi za uhai wake na kuiletea heshima kubwa klabu yake ya Simba na Taifa kwa ujumla, pale walipofanikiwa kuisukumiza nje ya michuano ya Afrika, klabu ya Zamalek ya Misri na kuivua ubingwa miamba hiyo ya soka ya kaskazini mwaka 2003.

Kiungo huyo aliyeanza kuvuma katika miaka ya 2000, amefariki dunia kutokana na kusumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa wa kifua kikuu (TB).

Marehemu Christopher Alex, alizaliwa Septemba 12, 1975, na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Uhuru na kumaliza katika shule ya Chamwino huko Dodoma mwaka 1993. Alianza kucheza mpira kwenye timu ya daraja la nne ya Chamwino Utd na baadaye daraja la tatu akiwa na kikosi cha Aston Villa nayo ya Dodoma.

Mwaka 1999-2001, aliitumikia klabu ya CDA ya Dodoma, kabla ya kutimkia klabu ya Reli ya Morogoro mwaka 2002, na baadaye kujiunga na Wekundu wa Msimbazi Simba. Marehemu ameacha mtoto mmoja aitwaye Alex.

Kasongo, kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya DRFA, wametoa ubani wa shilingi laki mbili (200,000/=) kwa familia ya marehemu na kuwataka mashabiki wa soka na watanzania kuungana katika kuifariji familia hiyo kwenye kipindi hiki kigumu cha majonzi.

No comments:

Post a Comment