KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, February 10, 2015

BEKI ALIYEMKABA KOO TAMBWE AFUNGIWA MECHI TATU



Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu beki George Michael Osei wa Ruvu Shooting kutokana na makosa ya kinidhamu aliyoyafanya akiwa uwanjani.

Osei ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumkaba na kumchezea kibabe mshambuliaji wa Yanga, Amisi Tambwe ambapo ni kinyume na mchezo wa kiungwana (fair play) ameadhibiwa kwa kuzingatia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo la 2012.

Mlalamikiwa alifika mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 9 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Nyoso alikiri kufanya na kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi mchezaji Maguri kwa kitendo hicho.

Akisoma uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa alisema Osei alipopewa nafasi ya kujitetea alikana kufanya kosa hilo na kudai magazeti yametengeneza picha hizo. TFF iliwasilisha ushahidi wa magazeti mawili ya Championi na moja la The Guardian kwa kuzingatia  Ibara ya 96(3) ya Kanuni ya Nidhamu ya TFF Toleo la 2012.

Katika uamuzi wake, Kamati imesema kitendo cha Osei ni kinyume na kanuni ya mchezo wa kiungwana (fair play), na kuongeza kuwa kanuni za TFF kwa makosa kama hayo ni dhaifu, hivyo kuagiza zirekebishwe ili ziweze kuwa kali zaidi.

Katika hatua nyingine Kamati hiyo, imetupa malalamiko yaliyowasilishwa na TFF dhidi Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona, na Katibu wa Simiyu (SIFA), Emmanuel Sorogo.

Kwa upande wa Sorogo, Kamati imesema baada ya kupitia vielelezo vya pande zote, hasa upande mlalamikiwa imeridhika kuwa hakushiriki katika kumpiga refa kwenye mechi ya Kombe la Taifa kwa Wanawake kati ya Shinyanga na Simiyu.

Badala yake aliyehusika ni Kocha wa Simiyu, Emmanuel Babu ambaye tayari uongozi umeshachukua hatua dhidi yake kwa kumsimamisha kwanza wakati akisubiri kufikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya SIFA.

Pia barua ya kumsimamisha kocha huyo ilitumwa kwa Katibu Mkuu wa TFF na Mkurugenzi wa Mashindano. Kamati imeyachukulia maneno ya mlalamikiwa kuwa ni sahihi ndiyo maana hayakupingwa na TFF, hivyo malalamiko dhidi ya mlalamikiwa hayana msingi na yametupwa.

Kwa upande wa Galibona ambaye ripoti za Kamishna na refa zilionyesha kuwa alishiriki kuhamasisha marefa kupigwa baada ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Polisi Mara FC na Mwadui FC, Kamati imesema mlalamikiwa aliwasilisha vielelezo vinne kuthibitisha kuwa hakuhusika.

Kamati imesema licha ya ripoti ya Saleh Mang'ola kumtaja Galibona, lakini maelezo ya refa huyo na msaidizi wake Rebecca Mulokozi waliyoandika Kituo cha Polisi baada ya tukio hilo hayakumtaja mlalamikiwa mahali popote.

Pia barua ya FAM kwenda TFF kuhusu matukio ya mechi hiyo yanamtoa hatiani mlalamikiwa, hivyo Kamati imeamuru kuwa malalamiko dhidi ya Galibona hayana msingi na yametupiliwa mbali.

No comments:

Post a Comment