KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 19, 2015

MSUVA AIPAISHA YANGA LIGI KUU, YAICHAPA PRISONS 3-0


YANGA jana iliendeleza wimbi la ushindi katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuicharaza Prisons mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.

Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kuendelea kujikita kileleni mwa ligi hiyo, ikiwa na pointi 28 na kuiacha kwa mbali kidogo, Azam, ambayo jana ililazimishwa kutoka suluhu na Ruvu Shooting.

Mshambuliaji Simon Msuva aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu.

Msuva alifunga bao la kwanza dakika ya tatu alipounganisha wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Coutinho.

Bao la pili la Yanga lilitokana na uzembe wa mabeki wa Prisons kujifunga wakati wakijaribu kuokoa shuti lililopigwa na Coutinho. Timu hizo zilikwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Msuva aliihakikishia Yanga ushindi dakika ya 62 baada ya kuifungia bao la tatu, akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Coutinho.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Azam ilibanwa mbavu na Ruvu Shooting baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu kwenye uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo wakati Simba itakapomenyana na Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

No comments:

Post a Comment