'
Wednesday, February 20, 2013
TYSON:NAMPENDA EVANDER HOLYFIELD
CHICAGO, Marekani
ILIKUWA kama filamu wakati mabingwa wa zamani wa ngumi za kulipwa za uzani wa juu, Mike Tyson na Evander Holyfield walipokutana kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16.
Safari hii hawakukutana kwenye ulingo wa ndondi. Walikutana katika uzinduzi wa kinywaji kipya uliofanywa na Holyfield katika grosari ya Jewel-Osco iliyopo mjini Chicago.
Kabla ya tukio hilo, Tyson (46) alimwendea Holyfield (50) kwa furaha na kumkumbatia. Ilikuwa kama vile marafiki waliopoteana zamani wanafurahia kukutana.
Muda wote wa tukio hilo, Tyson alionekana akitabasamu kwa furaha na kuonyesha meno nje wakati Holyfield alibaki akicheka.
Tukio hilo liliwakumbusha mashabiki wa ndondi pambano la kihistoria kati ya mabondia hao wawili lililofanyika Juni 1997 mjini Las Vegas, ambapo Tyson alimng'ata sikio Holyfield na kuondoka na kipande cha nyama.
Kwa sasa tukio hilo limebaki kuwa historia baada ya mabondia hao kuamua kumaliza tofauti zao na kuwa marafiki.
"Nilitaka kumuona Holyfield. Nampenda Evander. Nitaendelea kuwa karibu naye hadi mwisho wa maisha yangu,"alisema Tyson.
Kujitokeza kwa Tyson kumuunga mkono Holyfield katika uzinduzi wa kinywaji hicho kulionekana kama ni njia bora ya kusema samahani kwa bingwa huyo wa zamani wa masumbwi duniani.
Uzinduzi wa kinywaji hicho pia ulipambwa na mshindi wa medali ya dhahabu katika ndondi za uzani wa juu katika michezo ya Olimpiki ya 1984 iliyofanyika Los Angeles, Marekani.
Tyson, ambaye amecheza filamu kadhaa, ikiwemo The Hangover wakati alipokuwa kwenye chati, alikuwepo mjini Chicago kwa ajili ya kupromoti filamu yake mpya.
Filamu hiyo inaelezea maisha ya bondia huyo tangu alipokuwa mtoto wa mitaani katika mitaa ya Brooklyn hadi alipotwaa ubingwa wa dunia kabla ya kuporomoka.
"Hii inaonyesha ni jinsi gani ameamua kubadilika,"alisema Holyfield akimzungumzia Tyson.
"Nafikiri amewapa nafasi watu waelewe kwamba alifanya makosa na kilichotokea kimebaki historia. Amekubali ukweli huo na nimemsamehe. Hivyo ndivyo namna nzuri ya kujirekebisha katika maisha,"aliongeza Holyfield.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment