KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 14, 2013

SIKINDE YAPATA MDHAMINI MJERUMANI



Mpiga gita la solo maarufu nchini, Adolph Mbinga (kulia) akipiga ala hiyo wakati wa onyesho la bendi ya Mlimani Park Orchestra lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa klabu ya Sigara, Chang'ombe, Dar es Salaam. (Picha na Emmanuel Ndege).
BENDI ya muziki wa dansi ya Mlimani Park Orchestra (Sikinde) imepata mdhamini kwa ajili ya kurekodi baadhi ya nyimbo zake mpya na za zamani.

Katibu wa bendi hiyo, Hamisi Milambo alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mdhamini huyo ni Werner Grabner, ambaye ni raia wa Ujerumani.

Milambo alisema Werner amejitoleza kugharamia kurekodi nyimbo hizo kwa CD na video kwa lengo la kuitangaza bendi hiyo kimataifa.

Alisema Mjerumani huyo ni shabiki mkubwa wa Sikinde na amekuwa akiifuatilia bendi hiyo kwa miaka mingi.

Kwa mujibu wa Milambo, moja ya makubaliano waliyofikia na Werner ni kurekodi nyimbo za zamani za bendi hiyo na nyingine mpya.

Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya nyimbo za zamani, lakini alizitaja nyimbo mpya watakazozirekodi kuwa ni Nitalipa deni, Mkwezi, Nundule na Jinamizi la talaka

Wakati huo huo, Milambo amesema bendi yake imerejea kwenye ukumbi wa klabu ya Sigara kuanzia mwishoni mwa wiki iliyopita.

Milambo alisema jana kuwa, walisimama kufanya maonyesho kwenye ukumbi huo kutokana na wamiliki wake kuufunga kwa muda kwa ajili ya kuufanyia matengenezo.

Alisema katika onyesho la wikiendi hii, wamepanga kuwatambulisha wanamuziki wao wapya waliowaajiri hivi karibuni kwa lengo la kujiimarisha.

Milambo alisema wameamua kujiimarisha baada ya kuondoka kwa mwimbaji wao wa zamani, Athumani Kambi, aliyejiunga na Msondo Ngoma mwezi uliopita.

Katibu huyo wa Sikinde hakuwa tayari kutaja majina ya wanamuziki hao wapya, lakini tayari mpiga gita la solo wa zamani wa Twanga Pepeta na Mchinga Sound, Adolph Mbinga ameshaanza kuonekana kwenye maonyesho ya bendi hiyo.

"Kwa sasa bado tunamjaribu Mbinga iwapo ataweza kwenda na miondoko ya Sikinde. Kama atamudu, basi naye huenda akawa miongoni mwa wanamuziki wapya, tutakaowatambulisha Jumapili,"alisema.

Milambo alisema hawana wasiwasi na Mbinga kwa sababu ni mwanamuziki mzoefu na amewahi kupigia bendi kadhaa maarufu nchini.

No comments:

Post a Comment