'
Thursday, February 14, 2013
MATUMAINI: SIJAKATA TAMAA YA KUISHI
MSANII nyota wa vichekesho nchini, Tumaini Mwakibibi amesema, hajakata tamaa ya kuishi duniani licha ya kupatwa na maradhi yaliyotishia maisha yake.
Tumaini, maarufu kwa jina la Matumaini alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, hata alipokuwa Msumbiji, alijipa moyo na kuamini kwamba atapona.
"Niliona kama vile nitafia ugenini, lakini namshukuru Mungu kwamba baada ya kurejea nchini, nimepata matibabu hospitali ya Amana, hali yangu inaendelea vizuri na nimeruhusiwa kurudi nyumbani,"alisema.
Matumaini amewashukuru wasanii wenzake waliojitolea kwa hali na mali kuchanga pesa kwa ajili ya kumrejesha nchini na pia kumpeleka hospitali ya Amana kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Hata hivyo, Matumaini hakuwa tayari kueleza kiundani kuhusu matatizo yaliyompata alipokuwa Msumbiji, ambako alikwenda kwa ziara ya maonyesho.
Matumaini alirejeshwa nchini wiki iliyopita kwa ndege ya Shirika la Ndege la Msumbiji na kupelekwa moja kwa moja hospitali ya Amana, ambako alilazwa kwa siku mbili akipatiwa matibabu.
Aliporejeshwa nchini, msanii huyo hakuwa na uwezo wa kutembea na ilibidi abebwe na wasanii wenzake kwa ajili ya kuingizwa kwenye gari lililompeleka Amana.
Awali, Matumaini alikwenda kufanya maonyesho mkoani Mtwara, ambako promota mmoja kutoka Msumbiji alifurahishwa na maonyesho hayo na kuamua kumualika nchini kwake.
Kuna habari kuwa, baada ya kumaliza maonyesho yake nchini Msumbiji, Matumaini alianzisha uhusiano wa kimapenzi na promota huyo na kuamua kuishi naye.
Baadaye ilikuja kubainika kuwa, promota huyo alikuwa na mke, ambaye hakufurahishwa alipopata taarifa kwamba mumewe ameoa mke mwingine kutoka Tanzania.
Kuna habari kuwa, ulitokea mzozo mkali kati ya promota huyo na mkewe, ambaye aliahidi kumshikisha adamu Matumaini, ambaye alianza kuugua bila kujulikana maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.
Baada ya taarifa hizo kufika nchini, baadhi ya wasanii waliamua kuchangishana fedha kwa ajili ya nauli ya kumrejesha Matumaini na mpango huo ulitimia wiki iliyopita.
Akizungumzia hali ya msanii huyo, Rais wa Shirikisho la Wasanii Tanzania (TAFF), Simon Mwakifwamba alisema inaendelea vizuri na ameshatolewa hospitali ya Amana, ambako alilazwa kwa siku mbili.
Hata hivyo, Mwakifwamba alisema bado hajafahamu tatizo lililokuwa likimsumbua msanii huyo zaidi ya miguu yake kuvimba na kushindwa kutembea.
"Nadhani majibu ya ugonjwa wake yatapatikana baada ya siku chache zijazo, lakini kwa sasa anaendelea vizuri,"alisema.
Mwakifwamba alisema inavyoelekea, Matumaini hakupata matibabu mazuri wakati alipokuwa Msumbiji ndio sababu hali yake ilidhoofu.
"Kwa kweli, sisi kama shirikisho tumemsaidia sana, kuanzia kumrejesha nchini kutoka Msumbiji, kumpeleka hospitali na kumnunulia dawa. Hata familia yake imetushukuru sana kwa sababu haikuwa na uwezo wa kuyafanya yote hayo,"alisema.
Mwakifwamba alisema kilichosababisha Matumaini achelewe kurejea nchini ni muda wake wa kukaa Msumbiji kumalizika hivyo kukiuka sheria za uhamiaji za nchi hiyo.
Alisema ilibidi Matumaini alipishwe faini ya kuongeza muda wa kukaa nchini humo kabla ya kuruhusiwa kurudi nchini.
Rais huyo wa TAFF alisema tatizo hilo limekuwa likijitokeza kwa wasanii wengi nchini wanapokwenda kufanya maonyesho katika nchi za nje.
"Sisi wasanii tuna matatizo sana. Mara nyingi tunapokwenda nje kufanya maonyesho, tunajisahau. Muda wa viza zetu unapomalizika huku tukiwa hatujatimiza malengo yetu, hatufanyi taratibu za kuongeza muda. Tunaendelea kuishi kinyume cha sheria,"alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment