KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 7, 2013

K-SHER: DIAMOND NI KILA KITU



BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Khadija Shaaban 'K-Sher' ameibuka na kibao kipya kinachokwenda kwa jina la Nimechoka.

K-Sher, ambaye ni mama wa mtoto mmoja, amerekodi kibao hicho kwa kushirikiana na msanii nyota wa muziki huo nchini, Naseeb Abdul, maarufu kwa jina la Diamond.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, K-Sher alisema ameamua kumshirikisha Diamond kwa lengo la kukipa mvuto zaidi kibao hicho.

K-Sher amerekodi kibao hicho miezi michache baada ya kuipua kibao kingine kipya, kinachokwenda kwa jina la Hamu, ambacho alimshirikisha Lawrence Malima 'Marlaw'.

"Hiki ni kibao tofauti na vingine nilivyowahi kuvirekodi ndio sababu nimeamua kumshirikisha Diamond,"alisema.

K-Sher alisema ameamua kumshirikisha Diamond kwa sababu amewahi kufanyakazi na wasanii wengi maarufu wa muziki huo, hivyo anataka kuupa muziki wake sura tofauti.

"Diamond ni mwimbaji mzuri, ni platnums, anaimba vizuri, mstaarabu na ni kila kitu,"alisema K-Sher.

Mwanadada huyo alisema anaamini kibao chake hicho kitafanya vizuri sokoni na kuongeza kuwa, anatarajia kurekodi video yake hivi karibuni.

Kwa mujibu wa K-Sher, anatarajia kurekodi video hiyo chini ya usimamizi wa Adam Juma, ambaye amejizolea sifa lukuki kwa kurekodi video bora za muziki.

K-Sher alisema anataka video ya wimbo huo iwe ya kiwango cha juu na kuendana na matukio anayoyasimulia katika wimbo huo.

"Nimekuwa mpweke kwa muda mrefu, nahitaji ushirikiano kutoka kwa wasanii wengine,"alisema K-Sher na kuongeza kuwa, kibao chake hicho kipya kinaelezea matukio ya hivi karibuni yaliyokuwa kumkuta katika maisha yake.

K-Sher alikuwa kwenye likizo ndefu ya uzazi baada ya kujifungia mtoto wa kiume mwaka jana. Kabla ya kuamua kupumzika, mwanadada huyo alikuwa akitamba kwa kibao chake cha Uvumilivu, alichomshirikisha Tunda.

Mbali na kibao hicho, K-Sher pia aling'ara katika kibao cha Bado tunapanda, alichokirekodi akiwa na kundi la Tio Top Connection, lenye maskani yake Manzese, Dar es Salaam.

K-Sher alisema licha ya kuitwa mama na kukabiliwa na majukumu mengine ya ulezi wa mtoto na familia, hawezi kuachana na fani ya muziki kwa vile anaipenda na ipo kwenye damu yake.

“Kwanza namshukuru Mungu kwa kujifungua salama na kuweza kubeba dhamana ya kuitwa mama,hii itanifanya nizidi kujituma katika maisha yangu ili mwanangu aweze kuishi maisha mazuri hapo baadaye,” alisema.

K-Sher ni mmoja wa wasanii waliokuwa waking'ara katika kundi la Tip Top Connection kabla ya kuamua kujiengua mwishoni mwaka juzi kwa kile alichodai kuwa, ni kuiheshimu ndoa yake.

Wakati akijitoa kwenye kundi hilo, K-Sher alisema asingeweza kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja, akimaanisha mumewe na kundi lake.

Msanii huyo mwenye sauti maridhawa na umbo lenye mvuto alisema, si kweli kwamba aliondoka kwenye kundi hilo baada ya kutimuliwa kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini.

“Wakati nilipokuwa Tip Top Connection, nilikuwa peke yangu, sikuwa nimeolewa. Lakini kwa sasa mimi ni mama na mke wa mtu, napaswa kupanga mambo yangu mwenyewe,”alisema msanii huyo, ambaye mwanaye anajulikana kwa jina la Jam K.

“Nisingeweza kumudu kuendelea na muziki nikiwa Top Top Connection na wakati huo huo kuihudumia familia yangu kwa wakati mmoja, ndio sababu nimeamua kupiga muziki kwa kujitegemea ili niweze kupanga mambo yangu mwenyewe,”alisema.

K-Sher alikiri kuwa, yeye ni mmoja wa wasanii wachache wa muziki huo, ambao hawajawahi kukumbwa na kashfa ya aina yoyote na hiyo ni kutokana na kujiheshimu kwake mbele ya jamii.

Alisema malezi aliyoyapata kutoka kwa wazazi wake tangu akiwa mdogo yalifuata maadili ya kiislamu na ni watu wanaoheshimika, hivyo anapaswa kulinda heshima yao.

No comments:

Post a Comment