KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

PISTORIUS:SIKUPANGA KUMUUA MPENZI WANGU



JOHANNESBURG, Afrika Kusini

MCHEZAJI nyota wa michezo ya walemavu, Oscar Pistorius amesisitiza kuwa, hakuwa amedhamiria kumuua mpenzi wake, Reeva Steenkamp.

Pistorius alisema hayo juzi kupitia taarifa iliyosomwa mahakamani kuhusu tuhuma za kumuua Reeva katika tukio lililotokea nyumbani kwake Februari 14 mwaka huu.

Mshtakiwa huyo alidai kuwa, alimuua Reeva kimakosa kwa kuhisi ni mwizi aliyeingia nyumbani kwake kupora baada ya kushtuka kutoka usingizini usiku wa manane.

Awali, Mwendesha Mashtaka Gerrie Nel aliieleza mahakama kuwa, Pistorius aliamka kitandani na kuvaa miguu yake ya bandia na kutembea umbali wa mita saba kabla ya kumfyatulia risasi Reeva kupitia kwenye mlango wa bafu uliokuwa umefungwa.

Nel aliieleza mahakama kuwa, mauaji hayo yalikuwa yamepangwa na mtuhumiwa baada ya kutokea ugomvi kati yake na marehemu.

Lakini Pistorius aliieleza mahakama kuwa, alishtuka kutoka usingizini baada ya kusikia sauti kutoka bafuni, akiamini alikuwa mwizi.

Mshtakiwa huyo alidai kuwa, alipiga kelele kabla ya kufyatua risasi kupitia kwenye mlango wa bafu.

Alidai kuwa, baadaye aligundua kwamba Reeva hakuwepo kitandani na ikamjia hisia kwamba, huenda ndiye aliyekuwemo bafuni wakati huo.

Mshtakiwa huyo aliieleza mahakama kuwa, alilazimika kutumia kifaa cha kuchezea kriketi kuvunja mlango wa bafuni na kumkuta Reeva akiwa amelala sakafuni.

Pistorius alidai kuwa, alimkuta Reeva akiwa bado yupo hai na kuamua kupiga simu kuita gari la wagonjwa kabla ya mchumba wake huyo kupoteza maisha akiwa mikononi mwake.

"Nilishindwa kuelewa nitafunguliwaje mashtaka ya tuhuma za mauaji kwa sababu sikupanga kumuua mpenzi wangu,"alidai mwanamichezo huyo.

Kwa mujibu wa Pistorius, amekuwa na kawaida ya kulala na bastola kitandani kwake tangu alipopata vitisho vya kuuawa na kwamba alipoinuka kitandani kwenda bafuni, hakuwa amevaa miguu yake ya bandia.

Wakati taarifa hiyo ikisomwa mahakamani, Pistorius alikuwa akilia na kutetemeka.Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Desmond Nair.

Wakili Barry Roux, anayemtetea Pistorius aliieleza mahakama kuwa, Reeva hakuwa ameuawa kwa makusudi na kwamba zipo kesi nyingi za aina hiyo, ambazo baadhi ya watu waliwaua ndugu wa familia zao kupitia madirishani kwa kuwahisi wezi.

Pistorius alishinda medali mbili za dhahabu na moja ya fedha katika michezo ya Olimpiki ya Walemavu iliyofanyika 2012 mjini London, Uingereza.

Wakati huo huo, mazishi ya Reeva yalifanyika juzi nyumbani kwake katika mji wa Port Elizabeth.

No comments:

Post a Comment