KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

SIMBA YAUNGURUMA, AZAM YAFANYA MAUAJI


BAO lililofungwa na Amri Kiemba jana liliiwezesha Simba kutoka uwanjani na pointi zote tatu baada ya kuichapa Prisons bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini hapa.

Kiemba alifunga bao hilo dakika ya 36 kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Haruna Moshi 'Boban' aliyepiga krosi kutoka pembeni ya uwanja.

Ushindi huo umeiwezesha Simba kuendelea kujichimbia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 31 baada ya kucheza mechi 17 wakati Prisons ni ya 10 ikiwa na pointi 18.

Iliwachukua Simba dakika tano kufanya shambulizi kali kwenye lango la Prisons baada ya Mrisho Ngasa kupewa pasi ndani ya eneo la hatari na kubaki ana kwa ana na kipa David Abdalla, lakini shuti lake lilikuwa mboga kwa kipa huyo. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Prisons ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na nusura ipate bao dakika ya 59 wakati Fred Chudu alipoingia na mpira ndani ya 18, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Juma Kaseja.

Maafande hao waliendelea kulitia misukosuko lango la Simba dakika ya 61 na kulazimisha kona, lakini mabeki Juma Nyoso, Komabil Keita, Nassoro Cholo na Amir Maftah walikaa imara kuondosha hatari.

Simba: Juma Kaseja, Nassoro Cholo, Amir Maftah/Kigi Makasi, Komabil Keita, Juma Nyoso,Abdalla Seseme, Mrisho Ngasa/Haruna Chanongo, Amri Kiemba/Felix Sunzu, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Ramadhani Chombo.

Prisons: David Abdalla, Azizi Sibo, Laurian Mrale, Jumanne Elfadhil, Lugano Mwangama, Nurdin Issa, Sino Augustine, Fred Chudu, Emmanuel Gabriel, Elias Maguli na John Matei.

Wakati huo huo, Azam jana iliifanyia mauaji JKT Ruvu baada ya kuitandika mabao 4-0 katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiwezesha Azam kuzidi kukabana koo na Yanga katika uongozi wa ligi hiyo, baada ya kila moja kuwa na pointi 36, lakini zikiwa zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Yanga, ambayo ina mchezo mmoja mkononi, imefunga mabao 33 wakati Azam, iliyocheza mechi 17, imefunga mabao 31. Timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabao ya Azam yalifungwa na Khamis Mcha, aliyepachika wavuni mawili, Abdi Kassim 'Babi' na John Bocco.

No comments:

Post a Comment