'
Sunday, February 3, 2013
BAFANA BAFANA YATOLEWA KWA MATUTA
DURBAN, Afrika Kusini
WENYEJI Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana juzi walitolewa katika michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kufungwa kwa penalti 3-1 na Mali.
Mshindi wa pambano hilo la robo fainali, ilibidi apatikane kwa matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya bao 1-1.
Bafana Bafana ilikuwa ya kwanza kupata bao kipindi cha kwanza lililofungwa na Tokelo Rantie baada ya kupokea pasi kutoka kwa Thuso Phala.
Nahodha Seydou Keita aliisawazishia Mali kwa kiki ya umbali wa yadi sita iliyompita kipa Itumeleng Khune wa Bafana Bafana.
Katika kupigiana penalti tano tano, Bafana Bafana ilipoteza tatu, ikiwemo ya Lehlohonolo Majoro iliyopaa juu ya lango.
Pambano hilo lilikuwa na ushindani mkali huku wenyeji Bafana Bafana wakiwa wamepania kulipa kisasi cha kutolewa hatua kama hiyo na Mali katika fainali za 2002.
Bafana Bafana ilionyesha kiwango cha juu cha soka katika kipindi cha kwanza, lakini ukuta wa Mali ulikuwa makini kuondosha hatari zote.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Patrice Carteron wa Mali alikiri kuwa, wapinzani wao waliwaweka kwenye wakati mgumu hasa kipindi cha kwanza na kuwafanya walazimike kubadili mbinu kipindi cha pili.
Kocha Gordon Igesund wa Bafana Bafana alisema, licha ya kufungwa, vijana wake walionyesha soka ya kiwango cha juu na aliipongeza Mali kwa kushinda mchezo huo mgumu.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo iliyochezwa juzi, Ghana ilitinga nusu fainali baada ya kuichapa Cape Verde mabao 2-0.
Mabao yote mawili ya Ghana yalifungwa na Mubaraka Wakaso, moja kwa njia ya penalti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment