KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

SALIM AMIR, MKOBA WA TAIFA STARS ILIYOCHEZA FAINALI ZA AFCON 1980 (2)


WIKI iliyopita tulisoma wasifu wa mwanasoka mkongwe, Salim Amir, ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars kilichofuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za 1980 zilizofanyika nchini Nigeria pamoja na mtazamo wake kuhusu mwenendo na maendeleo ya mchezo huo kwa sasa. Endelea na sehemu hii ya mwisho ya mahojiano yetu na mchezaji huyo.

Salim alisema wakati alipokuwa kwenye kiwango cha juu kisoka, hakuwahi kufikiria kujiunga na mojawapo kati ya klabu kongwe nchini za Simba na Yanga kwa vile hakuona tofauti ya maisha ya wachezaji wake.

Alisema baadhi ya wachezaji aliokuwa nao Coastal Union kama vile Elisha John na Yanga Bwanga, waliwahi kujiunga na Yanga, lakini kutokana na kutopata mafanikio, waliamua kuondoka na kwenda Arabuni.

Licha ya kucheza soka kwa zaidi ya miaka 10, Salim alisema hakuna manufaa yoyote makubwa aliyoweza kuyapata kimaisha zaidi ya kujulikana na watu wengi na kutembelea nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya.

"Enzi zetu hakukuwa na manufaa yoyote tuliyoyapata zaidi ya kutembelea nchi nyingi. Hali haikuwa kama ilivyo sasa kwa wachezaji wetu,"alisema mkongwe huyo.

Alisema kufuzu kwa Taifa Stars kucheza fainali za Afrika za 1980 ni tukio pekee kubwa na ambalo hawezi kulisahau katika maisha yake kisoka. Anasema inasikitisha kuona kuwa, rekodi hiyo haijaweza kufikiwa na timu hiyo hadi sasa.

"Tulionyesha ushujaa mkubwa na kufanya kitu cha kihistoria, lakini hatukupata hadhi yoyote. Inawezekana ni kwa sababu ya uongozi wa wakati ule,"alisema.

Salim ameponda utaratibu unaotumiwa sasa na viongozi wa baadhi ya klabu za soka nchini kusajili wachezaji wengi wa kigeni wakati uwezo wao hauna tofauti kubwa na ule wa wazawa.

Alisema mchezaji bora wa kigeni ni yule mwenye uwezo wa kubadili sura ya mchezo wakati wowote atakapoingizwa uwanjani na si kama walivyo waliopo sasa.

Salim alisema ni vyema makocha wa timu za soka nchini wawe na utaratibu wa kufuatilia na kuibua vipaji vya wachezaji chipukizi na kuwaendelea badala ya kupapatikia wachezaji wa kigeni.

"Sipingi kuwepo kwa wachezaji wa kigeni hapa nchini kwa sababu uwepo wao unaweza kuleta changamoto kwa wachezaji wetu, lakini idadi yao inapaswa kupunguzwa,"alisema.

Salim alisema Tanzania inayo hazina kubwa ya vijana wenye vipaji vya kucheza soka, lakini bado hawajapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao kwa vile hakuna utaratibu wa kuwafuatilia.

Mkongwe huyo alisema mchezo wa soka kwa sasa ni kazi na iwapo utatumiwa vizuri, unaweza kuwapa manufaa mkubwa kimaisha wanasoka wa Tanzania na pia kuinua uchumi wa nchi.

"Lakini ili hayo yote yaweze kutimia, wanapaswa kuwa na malengo. Enzi zetu hakukuwa na huduma nzuri zinazotolewa kwa wachezaji kama ilivyo sasa, hii ni bahati kubwa kwao, hivyo wanapaswa kuitumia vizuri,"alisema.

Amezitaja mechi zilizo kwenye kumbukumbu ya maisha yake hadi sasa kuwa ni kati ya Taifa Stars na Zambia ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za 1980. Mechi hiyo ilichezwa 1979 mjini Dar es Salaam na katika mji wa Ndola.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars iliichapa Zambia bao 1-0 na ziliporudiana mjini Ndola, zilitoka sare ya bao 1-1.

"Ilikuwa mechi ngumu na ya kihistoria na iliyotuwezesha kuweka rekodi ya kufuzu kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza,'alisema Salim, ambaye katika mechi hizo alicheza nafasi ya beki wa kati akiwa na Jella Mtagwa.

Salim pia anaikumbuka mechi ya nusu fainali ya Kombe la Chalenji kati ya Taifa Stars na Malawi iliyochezwa 1979 nchini Uganda. Timu hizo zilitoka sare mara mbili kabla ya Taifa Stars kutolewa kwa mikwaju ya penalti.

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salim alisema wajumbe wa mkutano mkuu wa shirikisho hilo wanapaswa kuwa makini kwa kuchagua viongozi wenye sifa na uwezo.

Alisema viongozi wapya wa TFF wanapaswa kuweka mbele utaifa kwa kuwa na mipango madhubuti ya kuendeleza soka badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi.

"Ni miaka mingi sasa timu zetu hazijaweza kufika mbali kisoka katika michuano ya kimataifa. Lazima mkazo kwa viongozi wapya uwe ni kuinua soka ya Tanzania,"alisisitiza.

Salim ametoa mwito kwa wanasoka wa zamani nchini kujitokeza kuwania nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi wa klabu za soka, vyama vya soka vya wilaya, mikoa na taifa.

Alisema wakati umefika kwa TFF kuweka kanuni zinazotaka viongozi wa soka katika ngazi hizo, lazima wawe wamecheza soka na kuwa na uzoefu wa uongozi.

Ametoa mwito kwa TFF kuanzisha utaratibu wa kuwaendeleza na kuwapa mafunzo ya ukocha na uongozi, wanasoka wa zamani badala ya kuwaacha bila kuwatumia kuendeleza mchezo huo.

"Wapo baadhi ya wanasoka wa zamani, ambao walifika mbali kielimu. Hawa wanapaswa kutumika katika kuendeleza mchezo huo na ni watu muhimu,"alisema.

Salim alisema ni vyema pia kwa wanasoka hao wa zamani kupewa nafasi ya kuwa makamishna wa mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara na zinginezo kwa vile tayari wana uzoefu wa sheria za mchezo huo.

Mkongwe huyo wa soka alizaliwa 1953 katika mji wa Tanga. Alisoma shule ya msingi ya Jumuia na baadaye sekondari ya Usagara. Ana mke na watoto wanne, watatu wa kike na mmoja wa kiume.

No comments:

Post a Comment