'
Thursday, February 7, 2013
MPOTO KUWANIA UBUNGE 2015
MSANII nyota wa muziki na mashairi, Mrisho Mpoto ametangaza azma yake ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge wa 2015.
Mrisho alisema hayo wiki hii alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Amplifaya kilichorushwa hewani na kituo cha redio cha Clouds FM.
Msanii huyo alisema atagombea ubunge katika jimbo lolote, ambalo ataona mbunge wake analegalega.
"Ni wazo, ambalo limetoka kwa wananchi wenyewe wakisema nadhani tumekosea kupeleka mwakilishi, nadhani mwakilishi wetu ni wewe, kwa hiyo yale mahitaji ya wananchi yamekuwa makubwa, nikasema hapana, sasa lazima niende mwenyewe,"alisema Mpoto.
Aliongeza:"Nimekuwa mwakilishi wa wananchi kwa muda mrefu kupitia nyimbo zangu, lakini watu hawataki kusikia wala kubadilika. Tunapozungumzia maisha, tunazungumzia madirisha manne, kuna dirisha la kwamba wananchi wanajua wewe hujui, la pili mwananchi anajua wewe hujui, la tatu mwananchi hajui na wewe hujui, la nne wewe unajua, mwananchi anajua, kwa hiyo dirisha hili wawakilishi wetu wamekuwa wakitumia vibaya sana, wanafikiri wananchi hawajui wao ndio wanajua, ile dhana ya kuona wananchi hawajui ila wao ndio wanajua tunataka tukaionyeshe, tumezungumza sana,” Mpoto.
“Hebu angalia mfano mzuri wa pale Mtwara. Leo mpaka watu wanakufa mtu anasema siwezi kwenda kusaidia kule kwa sababu mimi mbunge wa jimbo lako, jimbo gani? Wewe ni mbunge wa wananchi, unapokuwa mbunge ni mbunge wa Watanzania wote. Watu hawataki kushughulika nao mpaka viongozi wanakuja kutoka huko ndio wanakwenda kule kuzungumza, haya mambo kama yanaweza kuzungumzwa yangetokea? Halafu unasema amekufa mtu mmoja tu, watu wawili? Ile pia ni roho, ile pia ni damu, tumeshindwa kusikilizwa hapa, tutasikilizwa tukiwa kulekule ndani?” Alihoji Mpoto.
Msanii huyo alisema tangu alipotangaza kuhusu azma yake hiyo, amepokea simu 80, zikiwemo 12 kutoka kwa wanasiasa pamoja na simu 400 kutoka kwa watu mbalimbali, ambao walimpongeza na wengine wakimuuliza maswali huku wabunge wakiongea naye kuhusu kujiunga nao.
Mpoto alikiri kuwa, anayo kadi ya chama kimojawapo cha siasa, lakini hakuwa tayari kutaja jina la chama hicho.
Alisema anatarajia kutangaza rasmi jina la chama hicho hivi karibuni na kusisitiza kuwa, wananchi wanahitaji vitu vitano tu ambavyo atavieleza wakati utakapofika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment