KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

MALKIA WA NYUKI KUMLIPA MILOVAN MIL 40/-


MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya klabu ya Simba, Rahma Al-Kharoos amejitolea kumlipa kocha wa zamani wa timu hiyo, Milovan Circkovic.

Milovan, ambaye aliinoa Simba msimu uliopita kabla ya kutemeshwa kibarua baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara, alikuwa akiidai Simba dola 24,000 za Marekani (sawa na sh. milioni 40).

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye hoteli ya Movenpick, Dar es Salaam, Rahma alisema amejitolea kumlipa kocha huyo kutokana na mapenzi yake kwa Simba.

Rahma, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Malkia wa Nyuki alisema, malipo hayo ni haki kwa kocha huyo kwa vile aliitumikia Simba.

“Sasa hivi kuna matatizo mengi, kwa hiyo timu haifanyi vizuri, wanachama hawajui waangalie nini, matatizo ya kocha wa zamani, ambaye hajalipwa pesa zake an waaangalie timu kwa nini haifanyi vizuri,”alisema.

Rahma alisema Simba lazima iondokane na hali hiyo na hakuna haja ya kuoneana haya wala kuogopana.

"Kuna watu wanaodhani mimi naburuzwa, ninachoweza kusema mimi siburuziki, nasema ukweli, kama tatizo lipo, litatuliwe,"alisema Rahma.

Makamu mwenyekiti huyo wa kamati ya fedha ya Simba alisema, tatizo lililopo sasa kwa klabu hiyo ni uongozi na amewashauri kukaa chini ya kumaliza tofauti zao.

Alisema madai ya kocha huyo yalikuwa ya msingi na lilikuwa ni suala la viongozi kukutana naye na kuyamaliza, lakini alishangaa kuona wakimkwepa.

"Nitampa kocha fedha zake kwa sababu ni haki yake, mtu katoka kwao amewafanyieni kazi, mpeni haki yake, kwa nini mnamzungusha," alisema mwanamama huyo.

Rahma alimtaka kocha huyo kucheki akaunti yake wiki ijayo na atakuta malipo hayo yakiwa yamefanyika kupitia benki.

No comments:

Post a Comment