KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 12, 2010

IVO MAPUNDA: Sina bifu na Kaseja




MMOJA wa makipa wanaotarajiwa kung’ara katika michuano ya soka ya mwaka huu ya ligi kuu ya Vodacom ni Ivo Mapunda wa African Lyon ya Dar es Salaam. Katika makala hii ya ana kwa ana, iliyoandikwa na Mwandishi Wetu, Athanas Kazige, kipa huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, anaelezea mikakati yake mbalimbali katika ligi hiyo.
SWALI: Kumekuwepo na taarifa kwamba umekuwa na bifu kwa muda mrefu na kipa Juma Kaseja wa Simba hata kufikia kutozungumza naye. Je, kuna ukweli wowote kuhusu jambo hili?
JIBU: Ukweli ni kwamba sina bifu lolote na kipa huyo kwani tuna mahusiano mazuri na mara nyingi huwa tunakuwa pamoja. Nina hakika hao wanaoeneza taarifa hizo wana malengo yao ya kutaka kutugombanisha.
Kuna wakati tulicheza pamoja katika timu ya Taifa Stars na tulishirikiana vizuri bila ya matatizo yoyote. Ninashangazwa sana na watu wanaoeneza uvumi huo. Mbali na hayo, naamini hizo ni siasa za mpira, kila mtu anaweza kuongea chochote kile ambacho anakiona kifanaa, lakini napenda kukuhakikishia kwamba sina ugomvi au bifu na Kaseja.
SWALI: Kocha mpya wa Taifa Stars, Jan Paulsen kutoka Denmark ametua nchini na tayari ameanza kukinoa kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mashindano ya kimataifa. Una maoni gani kuhusu ujio wa kocha huyo?
JIBU: Napenda kueleza bayano kuwa, kocha wa zamani wa Stars, Marcio Maxio alifanya mambo mengi mazuri hapa kiasi cha kuifanya Tanzania iwe gumzo ulimwenguni. Lakini yapo machache mabaya aliyoyafanya kama binadamu, inabidi asamehewe.
Binafsi nina imani kwamba Poulsen anaweza kutufikisha mbali zaidi kisoka kutoka pale alipoishia Maximo. Jambo la msingi ni kumpa ushirikiano kocha huyo ili aweze kutimiza malengo yake.
Ushirikiano huo unaweza kutolewa na wachezaji, viongozi, mashabiki na wadau wote wa soka kwa jumla, wakiwemo viongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa upande wangu, namshukuru sana Maximo kwa kuniita na kunipa nafasi ndani ya kikosi hicho. Niliweza kupata mafanikio makubwa nikiwa Taifa Stars, ikiwa ni pamoja na kusajiliwa na Yanga, St.Georges ya Ethiopia na African Lyon, ninayoendelea kuichezea hadi sasa.
SWALI: Unazungumziaje kuhusu uendeshaji soka nchini, unaofanywa na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania)?
JIBU: Napenda kuwapongeza viongozi wote wa TFF kwa kujitahidi kusaka maendeleo ya mchezo huo kwani tayari dira au mwelekeo wetu umeanza kujionyesha. Iwapo wataongeza juhudi zaidi, naamini tunaweza kufika mbali.
Sikatai kwamba zipo kasoro chache za kiuendeshaji kwa baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo, lakini ukweli unabaki palepale kwamba wameweza kufanya mambo makubwa kinyume na ilivyokuwa zamani, ambapo kila kukicha tulikuwa tukishuhudia malumbano na mapinduzi ya uongozi ndani ya TFF, hali iliyochangia kudorola kwa maendeleo ya mchezo huo.
Kasoro zilizopo sasa ndani ya TFF ni chache na iwapo zitafanyiwakazi na viongozi wa juu, naamini Tanzania itapiga hatua kubwa kimaendeleo nap engine kutimiza ndoto za kucheza tena fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Jitihada kubwa zinapaswa kuwekezwa katika mashindano ya vijana wa umri mbalimbali kwa sababu huko ndiko kwenye chimbuko la wanasoka wa baadaye wa Taifa Stars na klabu za Tanzania.
SWALI: Michuano ya ligi kuu ya Vodacom imepangwa kuanza Agosti 21 mwaka huu. Nini matarajio yako katika ligi hiyo?
JIBU: Nina hamu kubwa na ligi hiyo ili niweze kuonyesha uwezo wangu wa kucheza soka. Nimetumia muda mwingi kufanya mazoezi ili niwe fiti. Lakini kikubwa ni kwamba lengo langu ni kurudi tena kwenye kikosi cha Taifa Stars. Nataka kumshawishi Kocha Paulsen anirejeshe tena kwenye timu hiyo. Naamini kwa uwezo wa Mola, nitarejea tena kwenye timu hiyo.
SWALI: Kwa nini unakuwa na imani hiyo wakati msimu uliopita ulishindwa kuonyesha uwezo wako na kumshawishi Maximo akurejeshe kwenye timu hiyo?
JIBU: Zipo sababu nyingi zilizochangia mimi kushindwa kuonyesha makali yangu. Baadhi ya sababu hizo ni matatizo yaliyokuwa yakinikabili ya kudai haki zangu katika timu ya St.Georges baada ya kukatishiwa mkataba wangu pamoja na mambo mengine ya kifamilia.
SWALI:Hivi sasa una umri wako ni miaka 26. Nini matarajio yako katika mchezo wa soka, hasa katika msimu ujao wa ligi kuu?
JIBU: Kama nilivyosema awali, mawazo yangu bado yapo katika timu ya Taifa Stars. Nataka niendelee kuitumikia nchi yangu katika michuano ya kimataifa hadi pale nitakapostaafu kabisa kucheza mchezo huu. Imani yangu kubwa ni kwamba bado nina uwezo wa kuichezea Taifa Stars. Sidhani kama umri nilionao sasa ni kigezo cha mimi kuishiwa uwezo ama kushindwa kutimiza malengo yangu.
SWALI:Umejifunza nini kutokana na fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zilizofanyika hivi karibuni nchini Afrika Kusini?
JIBU: Nimejifunza mambo mengi sana, ikiwa ni pamoja na mbinu za kisasa za kudaka mipira. Kupitia fainali hizo, niliweza kuwashuhudia makipa wa nchi mbalimbali wakionyesha ufundi wa hali ya juu katika kulinda milango yao.
SWALI: Usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu huu wa ligi umeshamalizika. Je, kuna timu yoyote kubwa iliyokufuata kwa lengo la kukusajili?
JIBU: Zipo baadhi ya timu za nje ya nchi zilizoonyesha nia ya kutaka kunisajili, lakini mambo hayakuweza kukaa vizuri. Kwa upande wa hapa nchini, hakuna timu yoyote iliyyonyesha nia ya kunisajili.
SWALI: Unajisikiaje kuichezea timu ya African Lyon badala ya Simba au Yanga?
JIBU: Swali lako zuri sana ndugu yangu. Unajua unapokuwa unachezea timu kama Simba au Yanga, unakuwa mtu mwenye wakati mgumu kutokana na viongozi, wanachama na mashabiki kutokuwa na imani na wachezaji wao. Siku zote wanataka timu yao ishinde. Ikifungwa, inakuwa ni balaa kubwa.
Licha ya jambo hilo, timu hizo zina wapenzi wengi. Unakuwa maarufu na kujulikana kila kona, lakini timu inapofanya vibaya na bahati mbaya umechangia kufungwa, hapo utapata tabu sana, wewe pamoja na familia yako.

No comments:

Post a Comment