KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, August 18, 2010

Maproo wa Yanga hatarini kuikosa ligi

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), huenda likawazuia wachezaji wapya watano wa kigeni kuichezea Yanga katika msimu huu wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
TFF itafikia uamuzi huo iwapo Yanga itashindwa kuwalipa haki zao wachezaji wake wanne iliowaacha kwenye usajili wa msimu huu kabla ya mikataba yao kumalizika.
Wachezaji wa kigeni wa Yanga waliopo hatarini kuzuiwa kucheza ligi hiyo, inayotarajiwa kuanza keshokutwa ni Yaw Berko, Isaack Boakye, Kenneth Asamoah, Ernest Boakye na Ivan Knezevic.
Habari kutoka ndani ya TFF zimeeleza kuwa, shirikisho hilo limepanga kuwakutanisha wachezaji walioachwa kwenye usajili na uongozi wa Yanga ili kufikia muafaka wa malipo yao.
Kwa mujibu wa habari hizo, kikao hicho kimepangwa kufanyika leo kwenye ofisi za shirikisho hilo, ambapo TFF itawakilishwa na Kaimu Katibu Mkuu, Sunday Kayuni na baadhi ya wanasheria wake.
Wachezaji walioachwa na Yanga kabla ya mikataba yao kumalizika ni Wisdom Ndlovu, John Njoroge, Ali Msigwa na Steven Marashi.
Ndlovu na wenzake waliwasilisha malalamiko TFF wakipinga kuachwa dakika za mwisho huku mikataba yao na Yanga ikiwa haijamalizika.
“TFF imeitaka Yanga kumalizana na wachezaji hao kabla ya ligi kuanza Jumamosi, vinginevyo wachezaji wake wapya watano wa kigeni watazuiwa kucheza ligi,”kimesema chanzo cha habari.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alithibitisha jana kuhusu kuwepo kwa kikao hicho na kuongeza kuwa, anaamini suala la wachezaji hao litamalizwa siku chache zijazo.

No comments:

Post a Comment