KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 26, 2010

MARIAM CHOKORAA: Mwimbaji na mcheza shoo wa bendi ya Manchester

WACHEZA shoo wa bendi ya Manchester United wakiwa katika picha ya pamoja
MARIAM Chokoraa

KWA mashabiki wa muziki wa dansi waliowahi kuhudhuria maonyesho ya bendi ya Manchester yenye maskani yake Mbagala, Dar es Salaam, jina la Mariam Hassan si geni kwao. Ni mmoja wa waimbaji na wacheza shoo wanaoing’arisha bendi hiyo kutokana na uwajibikaji wake jukwaani.
Sauti yake ni maridhawa na yenye mvuto wa aina yake. Huimba kwa hisia na madoido ya aina yake. Lakini huvutia zaidi pale anapojumuika na wacheza shoo wa bendi hiyo kulishambulia jukwaa.
Licha ya kuwa na mwili uliojaa, ana uwezo wa kuuchezesha anavyotaka, akifuatisha mipigo ya ala na hivyo kuwafanya mashabiki watamani kumkodolea macho hadi mwisho wa onyesho.
Huyo ndiye Mariam, mwimbaji na mcheza shoo aliye maarufu zaidi kwa jina la Mariam Chokoraa, kufuatia kuolewa na mwimbaji nyota wa bendi ya Twanga Pepeta International, Khalid Chokoraa kabla ya kutengana.
Mariam (27) alifunga ndoa na Chokoraa mwaka 1999 na kuzaa naye mtoto mmoja wa kiume. Alikutana na Chokoraa walipokuwa mjini Tanga kwa shughuli za muziki kabla ya kuhamia naye katika bendi ya Extra Bongo mwaka 2003.
Mwanamuziki huyo hapendi kuzungumzia sana ndoa yake na Chokoraa na sababu za kuvunjika kwake. Kwake hiyo imebaki kuwa historia. Ni mambo ya zamani, hapendi na hataki kuyakumbuka.
Akizungumza na BURUDANI wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, Mariam alisema alianza kujihusisha na muziki kwa kucheza shoo katika promosheni za vinywaji mbalimbali mjini Tanga.
Alisema ni katika promosheni hizo, aliweza kukutana na Chokoraa na hatimaye wakaangukia katika dimbwi la mapenzi kabla ya kufunga ndoa na kuwa mume na mke.
Je, Mariam ndiye aliyeimbwa na Chokoraa katika kibao chake cha ‘Kuachwa’, alichokirekodi kwa kushirikiana na Charles Baba, Kalala Junior na Jose Mara?
Mariam hapendi kulizungumzia jambo hilo. Pia hayuko tayari kukubali ama kukataa ukweli juu ya kibao hicho.
“Nisingependa kuzungumzia jambo hilo, kama unaweza ni bora umuulize Chokoraa mwenyewe,”alisema mwanadada huyo.
Akiwa Extra Bongo, Mariam alikuwa akishiriki kucheza shoo kwenye maonyesho mbalimbali ya bendi hiyo kabla ya kuvunjika. Akaamua kubisha hodi Bicco Stars, ambako nako hakudumu muda mrefu kutokana na bendi hiyo kusambaratika.
Baada ya kuvunjika kwa Bicco Stars, mwanamama huyo aliamua kupumzika kwa muda shughuli za muziki huku akitafakari nini cha kufanya. Wakati huo, tayari Mariam alishakuwa ameachana na mumewe Chokoraa.
“Nilisimama shughuli za muziki kwa muda mrefu kabla ya kujiunga na SOT Band ya Tanga na baadaye Manchester Band, ambako ndiko niliko hadi sasa,”alisema Mariam.
Alisema ujio wake ndani ya bendi ya Manchester ulikuwa na neema kubwa kwa vile baada ya miezi michache tangu alipojiunga nayo, alikabidhiwa wadhifa wa kuwa kiongozi mkuu baada ya kiongozi wa zamani, kutimuliwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
“Japokuwa nipo na bendi hii kwa miezi michache, naamini ina uwezo wa kufika mbali kwa sababu viongozi wake ni waelewa, wapo imara na wanawathamini sana wanamuziki wao,”alisema.
Mariam alisema uchanga wao katika fani, kujituma na ari ya kupata mafanikio ni miongoni mwa mambo yanayowafanya wafanyekazi zao kwa umakini mkubwa ili waweze kupata mafanikio zao. Kwa sasa, bendi hiyo inajiandaa kuipua albamu yao ya kwanza, itakayokwenda kwa jina la ‘Urithi wa baba’. Albamu hiyo itakuwa na vibao sita na Mariam ameshiriki kuimba baadhi ya nyimbo.
Licha ya uchanga wake katika fani ya muziki, Mariam alisema havutiwi na tabia ya wanamuziki kuhamahama kutoka bendi moja hadi nyingine kwa kile alichadai kuwa, kunachangia kuua vipaji vyao.
Alisema ni kweli kwamba kuhama kwa wanamuziki kunalenga kutafuta maslahi mazuri zaidi, lakini alisisitiza ni vyema wadumu na bendi zao kwa muda mrefu.
“Sina hakika sana kama wanamuziki wengi wanaohama huwa wakitafuta maslahi kwa sababu wengine hurudi tena kulekule walikotoka. Sasa kama uliondoka katika bendi kwenda kutafuta maslahi, kwa nini unarudi tena kulekule?”Alihoji.
Aliwataka wanamuziki nchini waepuke tamaa kwa madai kuwa, ndiyo inayosababisha wahame kutoka bendi moja hadi nyingine. Alisema binafsi amekuwa akihamahama kutokana na bendi alizopitia kutoweka.
Ametoa mwito pia kwa wanamuziki nchini kuacha majungu na kuchukiana bila sababu. Alisema tabia za aina hiyo zimekuwa zikichangia bendi nyingi kusambaratika.
Mariam anavutiwa sana na uimbaji wa mwanamuziki Luiza Mbutu wa Twanga Pepeta International. Alisema anapenda siku moja afikie uwezo wa mwimbaji huyo mkongwe kwa wanawake hapa nchini.
Kiongozi huyo wa bendi ya Manchester alizaliwa miaka 27 iliyopita katika familia ya watoto wanne ya Mzee Hassan na Mama Mary. Katika familia yao, hakuna mtoto mwingine anayejihusisha na fani ya muziki. Alisoma shule ya msingi ya Girole ya Korogwe mkoani Tanga na kuishia darasa la saba. Hakuweza kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo wa kumuendeleza kielimu.

No comments:

Post a Comment