KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 14, 2013

SALIM AMIR, MKOBA WA TAIFA STARS ILIYOCHEZA FAINALI ZA AFCON 1980



KUMPATA Salim Amir katika mji wa Tanga haikuwa kazi ngumu. Kwa vile nilikuwa na namba yake ya simu, nilimpigia na baada ya kumpata, akanielekeza nyumbani kwake eneo la Makorola.

Licha ya umri wa miaka 60 alionao sasa, Salim bado ana nguvu na umbile lake halijabadilika. Ni lile lile alilokuwa nalo wakati alipokuwa akicheza soka. Ni mrefu wa wastani na bado mkakamavu.

Zaidi ya yote hayo, Salim ni mchangamfu na hupenda kuzungumza kwa sauti ya taratibu, lakini akiwa na hakika na kile anachokizungumza. Hutoa majibu ya swali analoulizwa bila ya kusita ama kujiuliza mara mbili.

Salim ni mmoja wa wanasoka wakongwe nchini, aliyejipatia sifa na umaarufu mkubwa kutokana na staili yake ya uchezaji. Ni mmoja wa mabeki waliokuwa wagumu kupitika, hasa alipokuwa akiunda ukuta wa katikati wa Taifa Stars akiwa na Jella Mtagwa.

Enzi zake, Salim aliwahi kuichezea Coastal Union ya Tanga kuanzia 1971 hadi 1980. Pia aliichezea timu ya Taifa, Taifa Stars kwa miaka saba kuanzia 1974 hadi 1980 alipoamua kustaafu soka baada ya kuumia goti.

Salim alipatwa na maumivu hayo wakati wa mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya Coastal Union na Simba iliyochezwa 1980 mjini Dar es Salaam. Tangu alipoumia, amefanyiwa operesheni ya goti mara tatu.

Mwanasoka huyo mkongwe alifanyiwa operesheni ya goti kwa mara ya kwanza 1985 kutokana na huduma hiyo kutokuwepo nchini wakati huo. Alifanyiwa tena operesheni hiyo mara mbili mwishoni mwa mwaka huo baada ya kubainika kuwa, goti lake halikuwa limekaa vizuri.

Salim ni mmoja wa wachezaji waliokuwa wakiunda kikosi cha Taifa Stars kilichofuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za 1980 zilizofanyika nchini Nigeria. Ilifuzu kucheza fainali hizo baada ya kuitoa Zambia.

Wachezaji wengine waliokuwa wakiunda kikosi hicho wakati huo niJuma Pondamali, Leopard Tasso, Mohammed Kajole,Ahmed Amasha, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.

Kikosi hicho kilichokuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama, kilicheza mechi tatu katika fainali hizo. Katika mechi ya kwanza, kilichapwa mabao 3-1 na wenyeji Nigeria, kikatoka sare ya mabao 2-2 na Ivory Coast kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri na kutolewa hatua ya makundi.

Salim aliitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza 1974 akiwa na Shiwa Lyambiko. Wakati huo, kikosi hicho kilikuwa chini ya kocha marehemu Marijani Shabani na kilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji.

Mwanasoka huyo mkongwe pia aliwahi kuichezea timu ya mkoa wa Tanga kwa zaidi ya miaka sita, ikiwa ni pamoja na kutwaa Kombe la Taifa 1973. Wanasoka wengine aliokuwa nao kwenye kikosi hicho ni Omar Mahadhi, Salehe Zimbwe, Mbwana Mtoto, Rashid Moyo, Mwabuda Muhaji, Hemed Mussa, Mohamed Makunda na wengineo.

Kwa sasa Salim bado anaendelea kujihusisha na mchezo wa soka, akiwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Coastal Union ya Tanga. Mkongwe huyo hakutaka kujihusisha na ukocha wa soka kutokana na kutokuwa fiti kiafya.

Akizungumza na Burudani mjini Tanga wiki iliyopita, Salim alisema kutokana na kufanyiwa operesheni ya goti mara tatu, hawezi kumudu mikikimikiki ya kukimbia uwanjani ama kutoa mafunzo kwa vitendo, kama ambavyo kocha anatakiwa kufanya kwa wachezaji.

"Huwezi kuwa kocha bila kuonyesha mafunzo kwa vitendo. Maumivu niliyoyapata yamesababisha nisiweze kuimudu kazi hiyo ndio sababu sikupenda kujihusisha nayo,"alisema.

Akizungumzia maendeleo ya mchezo huo nchini hivi sasa, Salim alisema yamedorola kutokana na wachezaji kutokuwa na ari na vipaji vya kucheza soka.

Alisema enzi zao, kiwango cha soka kilikuwa juu na wachezaji wengi walikuwa na vipaji vya aina yake vya kucheza soka na walicheza kwa ari kubwa na kujituma.

Salim alisema kwa sasa, vipaji vya wanasoka nchini vimepungua na si rahisi kuwapata wachezaji wa aina ya Sunday Manara na Mbwana Abushiri, ambao amewaelezea kuwa, walikuwa na uwezo wa kuufanya mpira wanavyotaka.

"Huwezi kuwalinganisha Jella Mtagwa na Sunday Manara na wachezaji wa sasa. Ipo tofauti kubwa,"alisema beki huyo wa zamani wa Taifa Stars.

"Wachezaji wa sasa wanalipwa fedha nyingi, lakini hawana ari. Wanashindwa kuelewa kuwa, mchezo wa soka kwa sasa ni kazi. Wanacheza soka bila kuwa na malengo,"alisema mkongwe huyo.

"Makocha wamekuwa wakijitahidi kutoa mafunzo, lakini wachezaji wanafanya vitu tofauti uwanjani. Inawezekana ni kutokana na uelewa mdogo,"aliongeza.

Salim alieleza kusikitishwa kwake kuona kuwa, tangu 1980, Taifa Stars haijaweza kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Alisema ilisikitisha zaidi kuona Taifa Stars ikifungwa nyumbani na Msumbiji katika mechi, ambayo ilikuwa ikihitaji ushindi ili iweze kufuzu kucheza fainali za 2008.

Mkongwe huyo wa soka pia alilaumu uongozi wa sasa wa mchezo huo nchini kuanzia katika ngazi ya klabu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba hauna malengo na mwelekeo.

Alisema viongozi wa zamani wa mchezo huo walikuwa wakielewa maana ya uongozi na walikuwa wakitumia busara zaidi katika kutoa maamuzi na kukaa vizuri na wachezaji, ndio sababu walipata mafanikio makubwa.

Salim alisema ni miaka mingi imepita bila Tanzania kufika mbali kisoka, hivyo ni vyema vyombo vinavyosimamia mchezo huo kutilia mkazo umuhimu wa kuinua kiwango cha mchezo huo.

"Naweza kusema kwamba, hivi sasa hatuko vizuri kisoka. Kila tukishiriki michuano ya Chalenji, tunatolewa mapema.

Itaendelea Alhamisi ijayo.

No comments:

Post a Comment