KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 28, 2013

WAGOSI WA KAYA HAIJAFA-DK. JOHN




JOHN EVANS 'DK. JOHN'


Asema walipigwa vita baridi ili kupunguzwa makali
Adai soko la bongo fleva limeoza na ni wizi mtupu

WAKATI wasanii John Evans 'Dk. John' na Fredy Maliki 'Mkoloni' walipounda kundi la Wagosi wa Kaya na kuibuka na albamu ya Ukweli mtupu, kila shabiki wa muziki wa kizazi kipya nchini alikiri kwamba kundi hilo lilikuwa moto wa kuotea mbali.

Hiyo ilitokana na baadhi ya vibao vyao vilivyomo kwenye albamu hiyo waliyoirekodi 2002 kama vile Tanga Kunani, Wauguzi, Trafiki, Kero na Soka ya Bongo, kutikisa anga ya muziki nchini.

Vibao hivyo vilitamba kutokana na sababu nyingi, lakini kubwa ni mpangilio wa ala za muziki na ujumbe uliomo kwenye nyimbo hizo, ambao uligusa maisha ya kila siku ya jamii.

Kundi hilo liliendelea kutamba 2003 baada ya kuibuka na albamu yao ya pili, inayojulikana kwa jina la Ripoti kamili kabla ya kuipua albamu ya tatu 2005, inayokwenda kwa jina la Nyeti. Albamu hizo zilirekodiwa kwenye studio za Master J zilizopo Dar es Salaam.

Kwa sasa, kundi hilo lililokuwa na maskani yake katika Jiji la Tanga, linaonekana kufa kimya kimya baada ya kushindwa kutoa albamu tangu 2006. Wasanii wa kundi hilo kila mmoja ameamua kufanyakazi kivyake.

Je, ni kipi kilichowasibu Wagosi wa Kaya? Ni kweli kundi hilo limesambaratika au bado lipo? Na ni kwa nini limesambaratika?

"Hili kundi bado lipo, halijasambaratika, isipokuwa limesimamisha shughuli zake kwa muda, lakini kurudi kwake itachukua muda mrefu,"alisema Dk. John alipozungumza na Burudani mjini Tanga hivi karibuni.

Dk. John alisema wameamua kusimamisha shughuli za kundi hilo kwa muda kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutingwa na shughuli binafsi na za kimaisha.

Aliitaja sababu nyingine iliyowafanya wasimamishe shughuli za kundi hilo kuwa ni mbinu chafu zilizokuwa zikifanywa na wapinzani wao kwa lengo la kuwamaliza.

"Zilifanywa mbinu nyingi kutushusha na kutumaliza kiusanii. Kulikuwa na vita baridi dhidi yetu bila sisi kujua,"alisema msanii huyo, ambaye katika nyimbo za kundi hilo alikuwa akiimba kwa sauti ya kisambaa.

"Ulifika wakati hata vyombo vya habari vilishiriki kutumaliza. Kila tulipokuwa tukipeleka nyimbo zetu kwenye vituo vya redio na televisheni, tulibaniwa,"aliongeza.

Kwa mujibu wa Dk. John, baadhi ya watangazaji wa redio na waandaaji wa vipindi vya muziki vya televisheni waliwalazimisha wawapatie pesa ndipo wapige nyimbo zao, lakini hawakukubaliana na jambo hilo.

Dk. John alisema walijaribu kutaka kulirejesha upya kundi hilo 2007, lakini walishindwa kutokana na kuendelea kwa vita hiyo baridi dhidi yao.

"Ni kuanzia wakati huo tukaamua kusimamisha shughuli zetu za muziki, mimi nikarejea Tanga, mwenzangu akabaki Dar es Salaam,"alisema.

Tangu wakati huo, Dk. John amekuwa akiendelea kujihusisha na muziki kwa kurekodi nyimbo zake binafsi wakati Mkoloni ameamua kujitosa kwenye ulingo wa siasa kwa kujiunga na CHADEMA.

Kibao chake cha kwanza kinajulikana kwa jina la Mashamsham ngoma ya Tanga, alichokirekodi 2008 kabla ya kuipua Mauzauza 2011. Kwa sasa, tayari Dk. John ameshakamilisha albamu inayojulikana kwa jina la Mashamsham, lakini alishindwa kuizindua kutokana na kukosa pesa.

Akizungumzia maendeleo ya muziki huo nchini, msanii huyo alikiri kuwa ni mazuri na makubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma, lakini nyimbo hazidumu kwa muda mrefu.

"Muziki hivi sasa ni biashara na una pesa nyingi kuliko ilivyokuwa enzi zetu. Tatizo pekee lililopo ni kwamba, nyimbo za siku hizi hazidumu kwa muda mrefu. Ikitoka leo, baada ya miezi minne inasahaulika,"alisema.

"Na hii ni kwa sababu wasanii tumekuwa wengi sana na kila mmoja anataka atoke. Na mwelekeo wa nyimbo zetu sote ni mmoja tu, mapenzi. Haiwezekani watu wote wauze nyanya," aliongeza.

Dk. John alisema wakati kundi lao lilipokuwa kwenye chati, walitegemea zaidi mauzo ya albamu kupata pesa kwa sababu idadi ya wasanii wa muziki huo ilikuwa ndogo ikilinganishwa na hivi sasa.

Alisema kwa sasa mauzo ya albamu yamekuwa mabaya kutokana na kukithiri kwa wizi wa kazi za wasanii, hasa kupitia kwenye mitandao.

Alisema msanii anaweza kurekodi albamu, lakini kabla hajaizindua, anakuta nyimbo zake zimeshavuja, watu wanazo kwenye simu na wengine wanaziuza kwenye CD. "Kwa jumla, mauzo ya albamu kwa sasa hayalipi,"alisema.

Dk. John alisema kinachowatoa wasanii hivi sasa ni maonyesho ya kwenye kumbi za burudani na matangazo ya biashara. Alisema hali hiyo ndiyo iliyowafanya wasanii wengi waamue kurekodi nyimbo moja moja kwa lengo la kujitangaza.

Alikiri kwamba ushindani katika muziki huo kwa sasa umekuwa mkubwa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya wasanii. Alisema msanii asiyekuwa makini katika kutunga na kurekodi nyimbo zenye ujumbe mzuri kwa jamii, hawezi kudumu muda mrefu.

"Hali hii ndiyo imesababisha baadhi ya wasanii waanze kushikana uchawi kwa sababu wengi hawajiamini. Wanakwenda kwa waganga wa kienyeji ili wapate dawa za kuwaletea mafanikio,"alisema.

Dk. John ameilaumu serikali kwa kushindwa kusimamia vyema biashara ya muziki na kusababisha ikose malipo ya kodi. Alisema kutokana na kukua kwa biashara hiyo, wakati umefika kwa serikali kudhibiti wizi wa kazi za sanaa.

Akitoa mfano, alisema baadhi ya watu wamekuwa wakianzisha studio za kurekodi muziki katika nyumba zao binafsi bila kufuata taratibu na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Alisema pia kuwa, mauzo ya albamu yamekuwa yakifanyika holela na kuwanufaisha wafanyabiashara wachache huku wasanii wakiendelea kunyonywa.
"Muziki ni uchumi kama ilivyo kwa madini na maliasili. Ukiwepo usimamizi mzuri, serikali itaingiza fedha nyingi,"alisema.

Dk. John alisema biashara ya muziki wa kizazi kipya kwa sasa ni wizi mtupu na soko lake limeoza ndio sababu wasanii wakongwe wamejikita zaidi katika kurekodi nyimbo moja moja na kufanya maonyesho kwenye kumbi za burudani badala ya kurekodi albamu.
"Hebu jiulize, AY na Mwana FA wamerekodi albamu kwa mara ya mwisho lini? Pengine utakuta 2005. Hawafanyi tena hivyo. Wameamua kurekodi nyimbo moja moja kwa lengo la kujitangaza ili wapate shoo,"alisisita.
Dk. John alisema iwapo maonyesho ya muziki wa kizazi kipya nayo yatakosa soko, utakuwa ndio mwisho wa wasanii na kwamba hali hiyo inaweza pia kuikuta fani ya filamu, ambayo ameielezea kuwa, utafika wakati nayo itakuwa hailipi.

No comments:

Post a Comment