KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, February 20, 2013

WENGER: MTANIKUMBUKA



LONDON, England

KOCHA Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger amejikuta akiwa kwenye wakati mgumu baada ya timu hiyo kutolewa na Blackburn Rovers katika michuano ya Kombe la FA.

Katika mechi hiyo ya hatua ya mtoano iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa Emirates, Arsenal ilichapwa bao 1-0 na Blackburn na hivyo kufungasha virago.

Kutolewa kwa Arsenal kulipokewa kwa hasira na mashabiki wa klabu hiyo, ambao wanaonekana dhahiri kumchoka kocha huyo na kutaka aondoke.

Mara baada ya Colin Kazim-Richards kuifungia bao Blackburn katika mechi hiyo, mashabiki wa Arsenal walilipuka mayowe wakisema 'Ondoka Wenger.

Kocha huyo aliwaambia waandishi wa habari baada ya mechi hiyo kuwa, wachezaji wake walizembea na kuchangia kipigo hicho.

Kocha huyo raia wa Ufaransa alisema timu yake iliyokuwa na wachezaji 11 wa kimataifa, ilimiliki mpira kwa asilimia 70, lakini uzembe wa mabeki wake ndio uliochangia kipigo hicho.

Je, ni wapi ambako Wenger atakwenda baada ya kuondoka Arsenal?

Hilo ndilo swali wanalojiuliza wachambuzi wa masuala ya soka nchini England baada ya kocha huyo kuwa amedumu Arsenal kwa zaidi ya miaka 16.

Baadhi ya wachambuzi wamemwelezea kocha huyo kuwa, ubahiri wa kusajili wachezaji nyota kwa bei mbaya, ndio umemponza kocha huyo na kuifanya timu hiyo ishindwe kutwaa taji lolote kwa misimu kadhaa.

Huu ni mwaka wa nane sasa Arsenal imeshindwa kutwaa taji lolote. Zipo sababu nyingi, lakini kubwa inaelezwa kuwa ni kushindwa kwa klabu hiyo kusajili wachezaji nyota.

Mwaka 2009, Arsenal ilimuuza Emmanuel Adebayo kwa klabu ya Manchester City kwa kitita cha pauni milioni 25 za Uingereza. Nafasi yake ilizibwa miezi 10 baadaye kwa kocha huyo kumsajili Marouane Chamakh, ambaye alisajiliwa kama mchezaji huru akitokea Bordeaux ya Ufaransa.

William Gallas naye aliihama Arsenal Agosti 2010 na kujiunga na Tottenham akiwa mchezaji huru. Siku nne baadaye, akasajiliwa Sebastien Squillaci kutoka Sevilla ya Hispania.

Mwanzoni mwa msimu uliopita, Cesc Fabregas, Samir Nasri na Gael Clichy nao waliondoka Emirates. Nafasi zao zilizibwa na  Mikel Arteta, Gervinho na Andre Santos.

Msimu huu, Robin van Persie aliondoka katika klabu hiyo na kujiunga na Manchester United kwa kitita cha pauni milioni 22. Nafasi yake ilichukuliwa na Olivier Giroud kutoka Montpellier ya Ufaransa, aliyesajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 13.

Katika wachezaji wote hao, Arteta ndiye ameonekana kuwa na mafanikio makubwa zaidi. Giroud alianza kuonyesha cheche zake baada ya kutua England wakati Santi Cazorla, Lukas Podolski, Thomas Vermaelen, Alex Oxlade-Chamberlain na Per Mertesacker wamejihakikishia namba za kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Wenger.

Lakini ukweli unabaki palepale kwamba, Wenger amepoteza wachezaji wengi wa kiwango cha dunia na kusajili wachezaji wa kiwango cha chini ama cha kawaida.

Msimu uliopita, kiungo Alex Song naye aliamua kufungasha virago na kujiunga na Barcelona na bado nafasi yake haijaweza kuzibwa hadi sasa.

Arsenal pia imeshindwa kuziba pengo la kipa Jens Lehmann, ambaye aliondoka katika klabu hiyo 2008 kabla ya kurudi kwa mkataba mfupi 2011.

Makipa wengine kama vile Manuel Almunia, Lukas Fabianski na Wojciech Szczesny wote wamepewa nafasi ya kuwania namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza kwa kutegemea uwezo wao.

Makipa hao watatu wameshindwa kukidhi matarajio ya Wenger, ambaye sasa atalazimika kusajili kipa mwingine wa kiwango cha juu iwapo ataendelea kuwepo Emirates msimu ujao.

Baadhi ya wachambuzi wa soka wameeleza kuwa, kushindwa kwa Wenger kuziba mapengo ya wachezaji wenye kiwango cha juu walioondoka kwa kusajili wachezaji wenye kiwango ndiko kulikochangia kuifanya timu hiyo ishuke kiwango.

Mapema wiki hii, Wenger alikaririwa akisema kuwa, amepanga kusajili nyota wapya kati ya watatu au wanne msimu ujao na kwamba atakuwa tayari kuvunja benki ili kuwapata nyota hao.

Pamoja na yote hayo, hakuna utetezi wowote, ambao Wenger anaweza kuutoa kwa sasa akaaminika. Anatambua wazi kwamba, hawezi kuomba msamaha akaeleweka.

Kinachowakera mashabiki wa Arsenal ni kwamba, iweje klabu kubwa na kongwe kama yao imalize misimu minane bila ya kutwaa taji lolote?

Akizungumzia shinikizo hilo la mashabiki, Wenger alisema watamkumbuka baada ya kuondoka katika klabu hiyo.

Wenger aliitetea rekodi yake katika klabu hiyo na kusema:"Nina hakika mtanikumbuka nitakapoondoka. Tazama timu ambazo nilipaswa kuzifundisha. Ipo siku nitawaeleza."

Kocha huyo aliwahi kupata ofa ya kuzifundisha timu za taifa za England na Ufaransa pamoja na klabu za Bayern Munich ya Ujerumanu, Real Madrid ya Hispania na Paris St Germain ya Ufaransa.

Wenger anakabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu baada ya kushindwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji lolote tangu 2005 ilipotwaa Kombe la FA.

"Nimekuwepo hapa kwa miaka 16 na ufundishaji wangu ni uleule,"alisema kocha huyo.

"Nimekuwa nikijihusisha na mchezo huu kwa miaka 30 na nimefanyakazi England kwa miaka 16 na ninastahili kuheshimiwa,"aliongeza.

"Mnaweza kusema nafanyakazi mbaya, lakini kunikashifu ni kosa. Watu wanasema silipi uzito Kombe la FA, lakini nimeshinda taji hilo mara nne. Mtaje kocha mwingine aliyetwaa kombe hilo mara nne. Ni upuuzi kusema napanga kikosi dhaifu kwa sababu tulianza na wachezaji 11 wa kimataifa,"alisema.

Wenger alisema Arsenal ndiyo timu pekee England iliyoweka rekodi ya kumaliza msimu bila kufungwa, imefuzu kucheza fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya mara moja na kufuzu kucheza nusu fainali na ameziita rekodi hizo kuwa ni za kujivunia.

 "Watu wanasema hatuwezo kushinda ubingwa wa Ulaya, lakini nafikiri hii ni nafasi nzuri kwetu kwa sababu nahisi ninacho kikosi imara,"alisisitiza.

No comments:

Post a Comment