KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, February 14, 2013

MALINZI AMSHUKIA TENGA



ALIYEKUWA mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemtaka rais wa sasa shirikisho hilo, Leodegar Tenga kuingilia kati sakata la kuenguliwa kwake kuwania nafasi hiyo.

Malinzi alitoa kauli hiyo mjini Dar es Salaam jana, alipokuwa akielezea msimamo wake baada ya Kamati ya Rufani ya TFF kumuengua kuwania urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Februari 24, mwaka huu.

Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Yanga alisema, hakubaliani na uamuzi huo wa Kamati ya Rufani ya TFF kwa vile sababu lizozitoa kuhusu kuenguliwa kwake hazina msingi.

Kamati hiyo, inayoongozwa na Iddi Mtigonjola, ilimuengua Malinzi kuwania wadhifa huo kwa madai kuwa, hana uzoefu wa uongozi wa miaka mitano na kukosa uadilifu kwa kupinga waraka uliotolewa na TFF wa kubadili katiba ya shirikisho Desemba mwaka jana.

Kamati hiyo ilipitisha jina la Athuman Nyamlani kuwa mgombea pekee wa kiti hicho, hatua iliyozusha malalamiko mengi kutoka kwa wadau wa soka nchini.

Malinzi alisema Tenga anayo nafasi kubwa ya kunusuru vurugu zinazoweza kutokea iwapo hatachukua hatua za kuhakikisha jina lake linarejeshwa katika uchaguzi huo.

"Mtu pekee ambaye anaweza kuleta amani na kuepusha vurugu zozote zile ni Tenga. Binafsi naamini ana uwezo mkubwa wa kuongoza. Namuomba aitishe mkutano wa dharura wa kamati ya utendaji kujadili suala hili," alisema Malinzi.

"Tenga amesifiwa kwa umahiri wake wa kuleta utulivu katika sekta ya mpira wa miguu Tanzania. Amesifiwa kwa kujenga taasisi imara, ambayo mhimili wake mkuu ni sekretarieti makini na kamati mbali mbali zilizo imara .

"Muda wa kuonyesha uongozi imara ni huu. Historia itamuhukumu kwa jinsi gani atasimamia suala hili. Haki sio lazima itendeke, lakini pia inatakiwa ionekane inatendeka. Kamati ya utendaji ya TFF inayo mamlaka ya kubatilisha maamuzi haya kwa maslahi ya mpira wa Tanzania,"alisema

Malinzi amewataka wadau wa soka nchini wawe watulivu wakati wakisubiri kupata ufumbuzi wa sakata hilo.

Akipangua hoja za mkata rufani wake, Agape Fue, Malinzi alisema 2008 aligombea nafasi ya urais na jina lake lilikatwa, lakini baada ya kukata rufani, alishinda na kuruhusiwa kugombea ambapo Tenga aliibuka kidedea.

Alisema aliambatanisha sifa na uzoefu wake katika uongozi wa soka ambapo aliwahi kuwa mjumbe wa Baraza la Michezo Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Michuano ya Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) na pia mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa wa Kagera.

Malinzi alisema aliwahi kuiongoza klabu ya Yanga akiwa katibu mkuu kati ya 2002 hadi 2005 na kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama Soka Mkoa wa Kagera.

Alisema hakubaliani na hoja ya kuvunja katiba ya TFF kwa kutumia waraka na kuongeza kuwa ataendelea kushikilia msimamo huo bila kubabaika.

Alisema Mkutano Mkuu wa TFF ndio wenye mamlaka ya mwisho ya kurekebisha katiba kwa kuwa ndiyo msingi mkuu wa undeshwaji wa shirikisho hilo.

Malinzi alisema hana sababu ya kuwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) kwa vile suala hilo liko ndani ya uwezo wa Tenga na kamati yake ya utendaji.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF jana ilisitisha kampeni za uchaguzi huo, kufuatia baadhi ya wadau wa soka kudai kuwa watakwenda mahakamani au kuleta vurugu iwapo jina la Malinzi halitarejeshwa katika uchaguzi huo.

No comments:

Post a Comment