MWIMBAJI nyota wa muziki wa dansi nchini na kiongozi wa bendi
ya Malaika, Christian Bella, amesema
sababu kubwa inayowafanya wanamuziki wa Tanzania kushindwa kupata mafanikio
kimataifa ni kukosa ubunifu.
Bella amesema wanamuziki wa Tanzania wanashindwa kwenda
na wakati na kwa miaka mingi sasa wamekuwa wakipiga muziki uleule, bila
kuubadili na kuweka vionjo vipya.
“Wanamuziki wa Tanzania hawataki kwenda na wakati,
wanakosa ubunifu. Wanataka kupiga muziki ule ule wa miaka ya 80,”amesema.
Bella, ambaye nyimbo zake nyingi zimetokea kugusa hisia
za mashabiki wa muziki nchini, alisema hayo wiki hii, alipokuwa akizungumzia
maendeleo yake kimuziki na hali ya muziki nchini.
Amesema licha ya kumiliki bendi ya Malaika, amekuwa
akirekodi nyimbo zake binafsi kwa lengo la kujitangaza na kukuza kipaji chake.
“Bendi ni yangu, lakini haiwezi kuimarika bila mimi kujitangaza,”amesema
mwanamuziki huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Amesema uamuzi wake huo hauna maana kwamba anaidharau
bendi hiyo au kuitelekeza, bali amepania kula sahani moja na wakali wa muziki
wa bongo fleva kama Ali Kiba na Naseeb Abdul ‘Diamond.
Amesema nyimbo zake zimekuwa zikipendwa na mashabiki
wengi wa muziki nchini kutokana na kuwa na mashairi yenye mvuto na pia kuweka
vionjo vipya mara kwa mara.
“Naimba na kupiga nyimbo zangu kwa kuchanganya aina
tofauti ya muziki. Nachanganya bongo fleva, dansi na pia naangalia wenzangu
wanafanya nini,”amesema Bella, ambaye aliwahi kuwa kiongozi wa bendi ya Akudo
Impact.
“Hakuna kipya katika muziki, aina zote za muziki
zinazopigwa sasa, zilishawahi kupigwa miaka ya nyuma.
“Hata Koffi Olomide na Fally Ipupa wanaiga vionjo vya
muziki vya Kitanzania. Katika muziki, hakuna kitu kinachoitwa kuiga muziki wa
bendi au mwanamuziki fulani,”amesema mwanamuziki huyo, ambaye amekuwa na
ushirikiano mkubwa na wasanii wa bongo fleva.
Bella amekiri kuwa binafsi anavutiwa na muziki wa kizazi
kipya kutokana na ukweli kwamba wasanii wake ni wabunifu na amekuwa akipata
vitu vingi kutoka kwao.
Mwimbaji huyo mwenye sauti yenye mvuto, inayopanda na
kushuka mithili ya mawimbi baharini, amesema baadhi ya wanamuziki wa Tanzania
hawapendi maendeleo ya wenzao na wamekuwa wakipenda kufuatilia maisha na kazi
za wenzao.
“Wapo wanaoweza kukufuatilia kila siku kutaka kujua
umefanya nini. Hata ukifanya kitu kizuri, utaona wanakukosoa, lakini ukiwaambia
waingie studio kurekodi, hawawezi,”amesema.
Bella amesema wakati alipoanzisha bendi ya Malaika,
baadhi ya wanamuziki walimponda na kumtabiria kwamba haiwezi kufika mbali,
lakini alijipa moyo.
“Ningekuwa na moyo dhaifu, ningekata tamaa mapema,
lakini nilijipa moyo kwamba nitafanikiwa, na kweli nimefanikiwa kwani bendi ipo
juu kuliko zile zilizoanzishwa miaka mingi,”amesema.
Amekanusha madai kuwa, amekuwa akiwabania wanamuziki
wenzake katika bendi ili wasipate umaarufu. Lakini amekiri kuwa msimamo wake ni
kwamba haiwezekani bendi ikawa na mastaa kibao. Amesisitiza kuwa staa katika
bendi huwa ni mmoja.
“Kila mtu anataka kuwa staa, hilo haliwezekani.
Mwanamuziki anaweza kuwa na nyimbo alfu moja kwenye kabati, lakini hakuna hata
moja iliyowahi kushika chati. Lazima wanamuziki watofautiane,”amesisitiza.
“Kama ni kweli nimekuwa nikiwabania wanamuziki wenzangu,
mbona baada ya kuondoka Akudo Impact, bendi imeshindwa kuendelea. Kwa nini wale
waliobaki wameshindwa kuiendeleza na kutumia nafasi ya kuondoka kwangu
kuonyesha vipaji vyao?” Alihoji.
Bella amesema katika bendi yake ya Malaika, hatoi ruhusa
kwa kila mwanamuziki kurekodi nyimbo zake binafsi kwa vile kufanya hivyo
kutaidhoofisha bendi.
Amesema kama suala ni kutaka kupata umaarufu, amekuwa
akiwaachia wanamuziki wake saa tatu kila wanapofanya maonyesho, kupiga nyimbo
za utangulizi ili kuonyesha makali yao kabla ya yeye kupanda stejini.
“Huwa tunaanza maonyesho yetu saa tatu usiku. Nawaacha
wanaimba kwa saa tatu, mimi naimba kuanzia saa sita usiku,” amesema.
“Umaarufu unaanzia kwenye maonyesho, sio kwenye TV. Wale
mashabiki wanaoingia ukumbini tangu saa mbili usiku ndio wanaokupa
umaarufu,”amesema.
Bella amesema kwa sasa anajiandaa kwa safari ya kwenda
Ufaransa kwa ajili ya kuingia mkataba na promota mmoja maarufu wa wanamuziki
kutoka DRC ili kurekodi nyimbo zake katika sura ya kimataifa na kujitangaza
zaidi duniani.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja jina la promota huyo na
pia kueleza lini anatarajia kwenda safari hiyo.
No comments:
Post a Comment