'
Sunday, May 3, 2015
YANGA YATOLEWA NA ETOILE YA TUNISIA KLABU BINGWA AFRIKA
Na Prince Akbar, SOUSSE
SAFARI ya Yanga SC katika Kombe la Shirikisho Afrika imefikia tamati usiku huu.
Hiyo inafuatia Yanga SC kufungwa bao 1-0 na wenyeji Etoile du Sahel katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse, Tunisia.
Kwa matokeo hayo, Yanga SC inatolewa kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya awali kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani Dar es Salaam. Etoile sasa watacheza na timu moja iliyotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania nafasi ya kupangwa katika makundi ya Kombe la Shirikisho.
Etoile walipata bao hilo kipindi cha kwanza, mfungaji Ammar Jemal, kwa kichwa akimalizia krosi ya Alkhali Bangoura dakika ya 24. Jemal aliurukia mpira uliompita kipa Deo Munishi ‘Dida’ akiwa peke yake pembezoni mwa lango na kuutumbukizia nyavuni kiulaini
Pamoja na Yanga SC kutangulia kufungwa, lakini walicheza vizuri na kukosa mabao kadhaa ya wazi.
Etoile ndiyo walioanza kulitia misukosuko lango la Yanga SC, baada ya Soussi Zied kushindwa kumalizia kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Tej Marouen dakika ya saba.
Kevin Yondan alifanya kazi nzuri dakika ya tisa baada ya kuokoa mpira ambao tayari ulikuwa umempita kipa wake, Dida uliopigwa na Soussi dakika ya tisa.
Dakika ya 18 Mouhbi Youssef alipoteza nafasi baada ya shuti lake kutoka nje kidogo kufuatia krosi ya Naguez Hamdi.
Yanga SC ilifanya shambulizi la kwanza dakika ya 26, lakini mpira wa kichwa uliopigwa na mshambuliaji Amissi Tambwe uligonga mwamba kufuatia krosi ya Juma Abdul.
Mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman alipiga juu ya lango dakika ya 33 baada ya kupokea krosi nzuri ya Mrisho Ngassa.
Etoile ilipata pigo dakika ya 42, baada ya kiungo wake tegemeo, Mcameroon Frank Kom kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Kom alionyeshwa kadi hiyo na refa Dennis Batte wa Uganda baada ya kumchezea rafu winga Simon Msuva, wakati tayari alikuwa ana kadi ya njano aliyoonyeshwa mapema dakika ya tisa kwa kumchezea rafu Ngassa.
Kipindi cha Yanga SC walikianza vizuri wakipeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Etoile, ambayo ilionekana dhahiri kuathiriwa na kupoteza mtu mmoja, tena muhimu, Kom.
Katika kuhakikisha wanaulinda ushindi, Etoile wakaanza kucheza mchezo wa kujihami na kufanya mashambulizi ya kushitukiza.
Hiyo iliwapa Yanga nafasi ya kutawala mchezo, lakini hawakuwa na madhara kwenye eneo la hatari la wapinzani wao hao.
Kikosi cha Etoile su Sahel kilikuwa; Aymen Ben Ayoub, Naguez Hamdi, Abdelrazek Ghazi, Boughattas Zied, El Jemmal Ammar, Frank Kom, Ben Amine, Bangoura Alkhaly, Tej Marouen, Mouihbi Youssef na Soussi Zied/Brigui Alaya dk48.
Yanga SC; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondan, Mbuyu Twite, Saidi Makapu, Simon Msuva, Salum Telela/Andrey Coutinho dk82, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Kpah Sherman/Hussein Javu dk65.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment