Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimeonyesha furaha yake baada ya timu tatu zilizo katika himaya yake, kumaliza katika nafasi za juu kwenye ligi kuu Tanzania Bara, iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamati ya Utendaji ya DRFA, chini ya Mwenyekiti wake, Almas Kasongo,imesema ni jambo la kufurahisha kuona mkoa wa Dar es salaam unafanya vizuri kisoka na kuwa mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine.
Timu hizo zimepongezwa kutokana na matayarisho waliyoyafanya tangu kuanza kwa msimu,ambapo mabenchi ya ufundi yameonyesha kuwa na nia ya dhati kuleta ushindani katika ligi.
Yanga na Azam ndizo zitakazoiwakilisha nchi katika michuano ya klabu barani Afrika,ambapo Yanga itakwenda huko kuwania kombe la klabu bingwa baada ya kutwaa uchampioni, huku Azam ikiwania kombe la Shirikisho baada kumaliza katika nafasi ya pili. Simba imemaliza katika nafasi ya tatu.
Aidha, DRFA imeipongeza TFF na kamati ya bodi ya ligi kwa usimamizi mzuri wa ligi msimu huu licha ya kuwepo na changamoto ndogondogo kwa klabu kulalamikia miundombinu ya vyumba vya kubadilishia nguo viwanjani na uonevu wa baadhi ya waamuzi.
DRFA imeishauri TFF kuangalia kwa kina na kuzifanyia kazi changamoto hizo zilizojitokeza msimu huu ili zisijirudie tena katika msimu ujao, kwa lengo la kuiboresha ligi ya Tanzania,ambayo kuanzia msimu ujao itakuwa na timu 16.
Pamoja na hayo DRFA imezishauri Yanga na Azam kujipanga vizuri kwa ajili ya mashindano ya klabu za Afrika msimu ujao, ili kuandika historia na kuleta vikombe hivyo kwa mara ya kwanza nyumbani.
No comments:
Post a Comment