'
Thursday, March 14, 2013
LYON, TOTO, POLISI ZACHUNGULIA KABURI
WAKATI michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara ikiwa inaelekea ukingoni, timu za African Lyon, Toto African na Polisi Moro zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.
Lyon inashika mkia katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi 20, ikifuatiwa na Toto African yenye pointi 14 na Polisi Moro yenye pointi 17.
Timu hizo tatu kila moja imesaliwa na mechi sita na hazina uwezo wa kushinda zote ili kujinusuru katika janga hilo la kuteremka daraja.
Iwapo Lyon itashinda mechi hizo sita, itafikisha pointi 31, Toto African itafikisha pointi 32 wakati Polisi Moro itafikisha pointi 35.
Timu nyingine, ambayo ikitereza inaweza kushuka daraja ni JKT Ruvu inayoshika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 19 baada ta kucheza mechi 19. Iwapo JKT Ruvu itashinda mechi zote zilizosalia, itafikisha pointi 37.
Wakati timu hizo nne zikipigana vikumbo kuepuka kushuka daraja, Yanga na Azam zinachuana vikali kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Yanga inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 45 baada ya kucheza mechi 19, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 37 na Simba yenye pointi 34.
Kwa sasa, Yanga inahitaji kushinda mechi nne ili iweze kuivua ubingwa Simba. Iwapo itashinda mechi hizo nne, itafikisha pointi 57, ambazo Simba haitaweza kuzipata.
Wakati huo huo, Yanga inaongoza kwa kufunga mabao katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Hadi sasa, Yanga imefunga mabao 36, ikifuatiwa na Azam yenye mabao 32 na Simba yenye mabao 28.
Coastal Union na Mtibwa Sugar zimefunga mabao 22 kila moja, zikifuatiwa na Kagera Sugar na Ruvu Shooting zilizofunga mabao 21 kila moja. JKT Oljoro imefunga mabao 20.
African Lyon ndiyo inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi baada ya nyavu zake kutikisika mara 32, ikifuatiwa na JKT Ruvu iliyofungwa mabao 30 na Toto African iliyofungwa mabao 28.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment