KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 14, 2013

FIFA YASITISHA MPANGO WA KULETA WAJUMBE WAKE TZ




SHIRIKISHO la Soka la Dunia (FIFA) limesitisha kwa muda mpango wake wa kutuma ujumbe nchini kuja kuchunguza kiini cha mgogoro uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, FIFA imeahirisha kutuma ujumbe wake hadi serikali itakapofikia mwafaka na shirikisho hilo.

"FIFA wamesema wameahirisha kuja hadi suala la serikali kuingilia kati masuala ya soka litakapopatiwa ufumbuzi,"alisema Wambura.

FIFA iliahidi kutuma wajumbe wake kuja nchini kuchunguza mgogoro huo baada ya baadhi ya wagombea walioenguliwa kuwasilisha malalamiko kwa shirikisho hilo wakipinga kuenguliwa kwao.

Hata hivyo, kabla ya FIFA kutuma ujumbe wake, serikali ilitangaza kuifuta katiba ya FIFA ya 2012 kwa madai kuwa, usajili wake ulifanyika bila kufuata taratibu.

Mbali na kufuta katiba hiyo, serikali iliitaka TFF iitishe mkutano wa marekebisho ya katiba na kuitisha uchaguzi mkuu kwa kufuata katiba ya 2006.

Hata hivyo, TFF imekuwa ikisita kutekeleza maagizo hayo kwa madai kuwa, katiba ya shirikisho hilo hairuhusu serikali kuingilia kati masuala ya soka.

TFF ilitoa waraka wiki hii kutoka kwa FIFA, ikitishia kuifungia Tanzania, iwapo serikali itaendelea kuingilia kati masuala yanayohusu soka.

Waraka huo ulieleza kuwa, FIFA imepata taarifa kupitia kwenye mitandao mbalimbali, zikieleza kuwa serikali imeitaka TFF ianze upya mchakato wa uchaguzi kwa kufuata katiba ya 2006.

Kupitia barua hiyo, FIFA imeeleza kuwa, nchi zote wanachama zinatakiwa kuendesha shughuli zake kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu kama ilivyoelezwa katika ibara ya 13 na 17 za katiba ya shirikisho.

Hata hivyo, waraka na maelezo hayo ya FIFA yamepingwa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala ambaye alisema wiki hii kuwa, serikali haiwezi kupokea maagizo kutoka shirikisho hilo kwa vile Tanzania ni nchi huru na yenye taratibu zake.

Makala alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa, iwapo Tanzania itafungiwa na FIFA, wanaopaswa kulaumiwa ni viongozi wa TFF kwa kutoa taarifa za upotoshaji kwa shirikisho hilo.

No comments:

Post a Comment