'
Sunday, March 24, 2013
NDANDA: MAONYESHO MATATU KWA WIKI HAYALIPI
KIONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Watoto wa Tembo International, Ndanda Kosovo amesema kwa sasa hana mpango wa kufanya maonyesho kila wiki kwa vile hayalipi.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Ndanda alisema ameamua kuja na staili mpya ya kufanya onyesho moja kila baada ya mwezi mmoja hadi mitatu ili kujipa sura ya kimataifa.
Ndanda alisema kufanya maonyesho matatu kwa wiki ni kujichosha na kwamba hakuna faida yoyote, ambayo wanamuziki wanaweza kuipata.
"Huko ni kutumika, kuanzia sasa nitafanya onyesho moja kila baada ya kipindi fulani, nikipata pesa natumia, zikiisha nafanya onyesho lingine,"alisema mwanamuziki huyo wa zamani wa bendi ya FM Academia
Ndanda alisema lengo lake ni kuwa kama baadhi ya wanamuziki maarufu barani Afrika kama vile Fally Ipupa, Koffi Olomide, JB Mpiana na Werrason.
Mwimbaji huyo anayependa kupaka rangi nywele zake alisema, wanamuziki wengi wa kiafrika wanaopiga muziki Arabuni, wamekuwa wakifanyakazi siku saba kwa wiki, lakini hakuna faida yoyote wanayoipata.
"Wanapiga muziki kuanzia Jumatatu hadi Jumatatu. Wanatumika wiki nzima, lakini hakuna faida yoyote ya maana wanayoipata,"alisema mwimbaji huyo, ambaye kuna wakati aliwahi kutamba kwa miondoko ya Wajelajela Origino.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za ushirikina katika muziki, Ndanda alisema haamini iwapo vitu hivyo vinafanyika kwa vile hapendi kuvifuatilia.
Alisema wakati alipokuwa katika bendi ya FM Academia, aliwahi kushutumiwa na baadhi ya wanamuziki wenzake kwamba anawafanyia ushirikina, lakini hakuwahi kufanya kitu kama hicho.
Ndanda alisema masuala ya ushirikina yanatokana na imani ya mtu na kwamba inawezekana wapo wanamuziki, ambao wamekuwa wakitegemea ushirikina katika kupata mafanikio.
Mwanamuziki huyo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) aliibuka na bendi ya Watoto wa Tembo International mwaka 2010.
Bendi hiyo ilikuwa ikiundwa na wanamuziki 18, wakiwemo waimbaji wanne, marapa wawili, wapiga vyombo sita na wacheza shoo watano. Mkurugenzi wa bendi hiyo alikuwa Jane Mawole.
Watoto wa Tembo ilikuwa ikifanya maonyesho yake kwenye hoteli zilizoko mbuga ya Mikumi mkoani Morogoro na kwenye baadhi ya hoteli za mjini Arusha.
Miongoni mwa vibao vilivyoitambulisha bendi hiyo ni pamoja na Afrika yetu, Usitoe mimba, Uniache, Kosovo Kiboko ‘Jambembe’ na Cecika. Bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki wake kwa kutumia miondoko ya Lilolo na Swala-k-Lakaswa.
Licha ya kupata umaarufu katika bendi ya FM Academia, Ndanda hana uhusiano mzuri na wanamuziki wa bendi hiyo, hasa kiongozi wake, Nyoshi El-Saadat.
Wanamuziki hao wawili wamekuwa wakitoleana lugha za kukashifiana mara kwa mara huku kila mmoja akijigamba kuwa juu ya mwenzake.
Ndanda pia aliwahi kukaririwa akisema kuwa, hana muda wa kusikiliza nyimbo za bendi za Kitanzania kwa kile alichodai kuwa, hazina ubunifu.
"Sina bifu na wanamuziki wa FM Academia ama Akudo Impact, lakini ukweli ni kwamba muda mwingi huwa napenda kusikiliza nyimbo za wasanii wa nje kwa vile wanafanya kweli katika muziki,"alisema.
"Sijawahi kusikiliza nyimbo za Akudo ama FM Academia kwa sababu ubunifu ni sifuri. Siwapondi wala sizungumzi hivi kwa nia mbaya, huu ndio ukweli wenyewe,"aliongeza.
Kuna wakati Ndanda aliwahi kwenda Marekani, ambako aliishi kwa zaidi ya miaka miwili akiwa anapiga muziki na bendi mbalimbali zinazoundwa na wanamuziki wa kiafrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment