KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 8, 2013

YANGA, TOTO AFRICAN DIMBANI KESHO DAR



MICHUANO ya Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Machi 9 mwaka huu) kwa mechi mbili ambapo vinara Yanga watakuwa wenyeji wa Toto Africans kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Mwamuzi wa mechi hiyo namba 135 atakuwa Andrew Shamba kutoka Pwani akisaidiwa na Abdallah Mkomwa na Abdallah Rashid pia wote kutoka Pwani. Kamishna ni Salim Singano kutoka Tanga wakati Mtathmini wa waamuzi ni Alfred Lwiza.

Nayo Polisi Morogoro itakuwa mgeni wa Azam kwenye Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Azam katika mechi hiyo namba 136 na nyingine mbili zinazofuata itakuwa bila kocha wake Steward John Hall ambaye Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu.

Charles Komba kutoka Dodoma ndiye atakayekuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 136 itakayochezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 10 mwaka huu) ambapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utashuhudia mechi kati ya Simba na Coastal Union ya Tanga. Waamuzi wa mechi hiyo ni Martin Saanya akisaidiwa na Jesse Erasmo na Vicent Mlabu wote kutoka Morogoro.

No comments:

Post a Comment