KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 14, 2013

DIAMOND KUJENGA MSIKITI DAR



MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' ameeleza nia yake ya kutaka kujenga msikiti katika Jiji la Dar es Salaam.

Diamond alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, kwa sasa anatafuta eneo zuri kwa ajili ya kujenga nyumba hiyo ya ibada.

Msanii huyo alisema amefikia uamuzi huo kwa lengo la kutekeleza imani yake katika dini ya kiislam, ambayo inawataka watu wenye uwezo kujitolea kujenga nyumba za ibada.

"Sijajua ni wapi nitakapojenga msikiti huo kwa sababu bado sijapata eneo. Hivyo kwa sasa natafuta eneo zuri linalofaa kwa shughuli hiyo,"alisema msanii huyo, ambaye amewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki za Kilimanjaro.

Uamuzi huo wa Diamond umekuja siku chache baada ya kukaririwa hivi karibuni akisema kuwa, amemjengea nyumba mama yake yenye thamani ya sh. milioni 60.

Mbali na kumjengea nyumba mama yake, Diamond alisema pia kuwa, amenunua gari jipya, ambalo ameliagiza nchini Japan. Alisema gari hilo ni tofauti na Prado VX analotumia sasa.

Wakati huo huo, Diamond ameamua kufuta ziara yake ya maonyesho ya muziki nchini Ujerumani.

Diamond ameeleza kupitia blogu yake wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo kutokana na promota wa ziara hiyo kushindwa kutimiza mahitaji yake.

Aliyataja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni pamoja na kushindwa kulipa pesa za maonyesho yaliyotakiwa kufanyika Machi 9 na 15 mwaka huu mjini Stuttgart, Ujerumani na Rotterdam, Uholanzi.

"Mimi na timu yangu nzima ya Wasafi hatutahudhuria kwenye maonyesho hayo," alisisitiza.

Diamond alisema alikuwa akipata maswali mengi kutoka kwa mashabiki kuhusu ziara hiyo, lakini aliamua kukaa kimya kwa sababu hakuwa na uhakika na waandaaji.

No comments:

Post a Comment