'
Sunday, March 24, 2013
VICENT KIGOSI 'RAY' : WATOVU WA NIDHAMU HAWANA NAFASI BONGO MOVIE UNIT
MSANII nyota wa filamu nchini, Vicent Kigosi 'Ray' amesema wameamua kuunda klabu ya Bongo Movie Unit kwa lengo la kusaidiana katika shida na raha.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Ray alisema wanachama wa klabu hiyo ni wasanii wa fani ya filamu wanaofuata na kuzingatia maadili ya uanachama.
Ray, ambaye ni mwenyekiti wa klabu hiyo alisema, awali ilikuwa ikiundwa na wasanii wachache, lakini baadaye waliamua kupanua wigo kwa kuwashirikisha wasanii wote wa fani hiyo.
Alisema lengo la klabu hiyo ni kuwa na wasanii wenye nidhamu na wanaofuata maadili na kuongeza kuwa, watakaokwenda kinyume watatimuliwa.
Ray alisema hawakuweza kumsaidia msanii mwenzao, Matumaini tangu alipokuwa akiugua nchini Msumbiji hadi aliporejeshwa nchini kwa sababu suala lake lilikuwa likishughulikiwa na Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF).
"Lakini wapo baadhi yetu wanachama wa Bongo Movie Unit, ambao tuliamua kumsaidia mmoja mmoja,"alisema.
Akizungumzia tatizo la baadhi ya wasanii wa kike kupenda kuvaa nusu uchi, Ray alisema inategemea ni katika mazingira gani.
Alisema kama msanii anacheza filamu inayozungumzia vitendo vya umalaya, ni lazima avae mavazi ya aina hiyo, lakini kama anafanya hivyo nje ya kazi, anakuwa na lake jambo.
"Unajua baadhi ya wasanii wa kike wameingia kwenye fani hii kwa lengo la kuuza sura. Wanataka waonekane kwenye filamu ili wapate wanaume wa kuwaoa ama kuwapa fedha ili wapate nyumba na magari. Hawa ndio wanaotuharibia fani yetu,"alisema.
Hata hivyo, Ray alivilaumu baadhi ya vyombo vya habari hasa magazeti ya udaku kwamba, vimekuwa vikiwachafua wasanii kwa makusudi kwa lengo la kuuza magazeti yao.
"Mimi sioni sababu kwa nini vyombo vya habari vifuatilie maisha binafsi ya msanii anapokuwa sehemu ya starehe. Huku ni kushusha heshima ya wasanii,"alisema.
Ray alisema uamuzi wao wa kujichuja katika klabu ya Bongo Movie Unit umelenga kujenga heshima ya wasanii wa fani hiyo na pia kuondokana na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Akitoa mfano, alisema hivi karibuni waliamua kumsimamisha uanachama Jacqueline Pentzel baada ya kukiri makosa aliyoyafanya na kuomba radhi.
Alisema si kweli kwamba wamemtimua msanii huyo kwenye klabu yao bali bado wanatafakari hatua za kuchukua dhidi yake.
"Kumtimua mwanachama katika klabu yetu si kumrekebisha. Dawa ni kumuweka sawa ili ajirekebishe,"alisema.
Ray alisema kazi ya kucheza filamu ilikuwa ikichukuliwa kuwa ni ya watu wasio na elimu, lakini hivi sasa imekuwa kivutio kwa wasomi, ambao wameanza kumiminika kwa wingi kuicheza hivyo inapaswa kuheshimiwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment