KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 11, 2013

RAZAK YUSUF , MWANASOKA MKONGWE ALIYEFANANISHWA NA CARECA WA BRAZIL



JINA lake halisi ni Razak Yusuf. Lakini alikuwa maarufu zaidi kwa jina la Careca, alilobatizwa na mashabiki wa soka wa mkoani Tanga kutokana na uwezo wake wa kucheza soka, uliofanana na mwanasoka huyo wa Brazil.
Hata hivyo, Razak hakuwa akilifurahia jina hilo. Alitaka Careca ndiye aitwe Razak kwa kile anachoamini kwamba, uwezo wake kisoka ulikuwa mkubwa zaidi kuliko aliokuwa nao mwanasoka huyo wa zamani wa Brazil, aliyestaafu soka akiwa na umri wa miaka 40.
Jina halisi la Careca lilikuwa Antônio de Oliveira Filho. Alikuwa mmoja wa wanasoka nyota wa Brazil waliocheza kwa mafanikio makubwa miaka ya 1980. Alikuwa na kipaji cha aina yake katika kufunga mabao. Baadhi ya klabu alizochezea ni pamoja na Sao Paulo ya Brazil na Napoli ya Italia.
Nyota ya Razak kisoka ilianza kung'ara 1985 alipojiunga na Coastal Union akitokea African Sports. Aliichezea Coastal Union hadi 1991 alipojiunga na klabu ya Simba. Alikuwa mmoja wa wachezaji walioiwezesha Simba kucheza fainali ya Kombe la CAF 1993.
Razak pia ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Coastal Union kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara 1988 na kupata nafasi ya kucheza michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati na Kombe la Washindi.
Baadhi ya wachezaji aliokuwa nao katika kikosi hicho ni Mohamed Mwameja, Hamisi Makene, Saidi Korongo, Douglas Muhani, Yassin Napili, Idrisa Ngulungu, Ally Maumba, Kassim Mwajeki, Mohamed Kampira, Kasa Mussa, Juma Mgunda, Hussein Makwuruzo, Aggrey Chambo na Riffat Saidi.
Kikosi hicho cha Coastal Union kilichokuwa chini ya makocha Zakaria Kinanda (sasa marehemu) na Joel Bendera, kilifuzu kucheza fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati na kufungwa na Breweries ya Kenya mabao 3-0. Michuano hiyo ilifanyika mjini Nairobi, Kenya.
Kufungwa kwa Coastal Union katika mechi hiyo ya fainali kulitawaliwa na mizengwe mingi. Kwanza walichezeshwa mechi ya nusu fainali dhidi ya AFC Leopards nyakati za usiku, ikiwa ni siku moja kabla ya fainali. Katika mechi hiyo, waliibuka na ushindi kwa njia ya matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya bao 1-1.
Wachezaji wa Coastal Union walilazimika kutolewa uwanjani saa saba usiku ili kuwaepusha na vurugu za mashabiki wa AFC Leopards. Walipofika kwenye hoteli waliyofikia, ilikuwa Ijumaa saa tisa usiku. Walipumzika kwa saa chache kabla ya kurudi uwanjani kucheza na Breweries katika mechi ya fainali.
Razak pia alikuwemo kwenye kikosi cha Coastal Union kilichocheza na Costa do Sol ya Msumbiji katika michuano ya Kombe la Washindi 1989. Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Coastal Union ilichezea kichapo cha mabao 3-2 kabla ya kupata kipigo kingine cha mabao 2-1 mjini Maputo.
Mwanasoka huyo mkongwe pia alikuwemo kwenye kikosi cha pili cha timu ya Tanzania Bara 'Kakakuona' kilichocheza michuano ya Kombe la Chalenji 1991 na kutinga fainali, ambapo kilichapwa bao 1-0 na Uganda.
Katika michuano hiyo iliyochezwa katika miji ya Mwanza na Arusha, Kakakuona ilyokuwa ikiundwa na wachezaji wengi chipukizi, ilijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa wa kucheza soka. Katika mechi za awali, ilitoka sare ya bao 1-1 na Uganda kabla ya kuichapa Shelisheli mabao 2-0.
Razak pia alikuwemo kwenye kikosi cha Simba kilichotinga fainali ya Kombe la CAF 1993 na kufungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya timu hizo kutoka suluhu katika mechi ya awali iliyopigwa mjini Abidjan.
Hata hivyo, Razak alicheza mechi chache za hatua ya awali ya michuano hiyo na kuumia. Alikuwa mmoja wa wachezaji walionyimwa zawadi ya magari waliyoahidiwa na mfadhili wao, Azim Dewji, kwa kile ambacho hadi sasa anashindwa kukielewa.
Akizungumza na Burudani kwenye uwanja wa Popatlal mjini Tanga hivi karibuni, Razak alisema alilazimika kustaafu soka 1993 kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
"Wakati ule hakukuwa na utaalamu wa tiba ya ugonjwa huo. Nililazimika kuacha soka bila kupenda nikiwa bado nina uwezo mkubwa,"alisema Razak, ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara na pia mmoja wa maofisa wa benchi la ufundi la Coastal Union.
Miongoni mwa mechi, ambazo Razak hawezi kuzisahau katika maisha yake ni ile iliyozikutanisha Coastal Union na AFC Leopards katika nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati 1988 nchini Kenya.
"Ilikuwa mechi ngumu, nzuri na kali. Mimi ndiye niliyefunga bao la Coastal Union. Nilifunga bao hilo kwa shuti kali la mbali. Lilikuwa bao zuri sana,"alisema.
Kinachomfanya Razak aendelee kuikumbuka mechi hiyo ni ukali wa AFC Leopards wakati huo, hasa baada ya kuzifunga Simba na Yanga katika mechi za kirafiki zilizochezwa mjini Dar es Salaam, lakini baadaye ikakubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Coastal Union mjini Tanga.
"Kocha wao, ambaye alikuwa raia wa Ghana, alitutabiria mapema kwamba tungetwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati na kweli tulifika mbali, lakini tulifungwa na Breweries katika fainali,"alisema mkongwe huyo.
Akizungumzia kiwango cha soka nchini hivi sasa, Razak alisema hakiridhishi kwa sababu mpira umegeuzwa zaidi kuwa mchezo wa kibiashara kwa wachezaji na viongozi. Alisema wachezaji wa sasa hawana ari na hawachezi kwa kujituma kama ilivyokuwa enzi zao.
"Zamani hakukuwa na pesa, lakini wachezaji walicheza kwa ari na kujituma. Lakini kikubwa zaidi ni kwamba walikuwa na vipaji vya kucheza soka, tofauti na ilivyo sasa,"alisema.
Razak pia amelalamikia maumbile ya sasa ya wanasoka wa Tanzania kwamba hayapo kisoka. Alisema wachezaji wengi wana maumbile madogo na hivyo kushindwa kuhimili ushindani wa timu pinzani, hasa kutoka nchi za Magharibi na Kaskazini mwa Afrika.
"Hebu tazama Taifa Stars ya 1981 iliyocheza fainali za Afrika kule Nigeria. Karibu wachezaji wote walikuwa na maumbile makubwa. Tazama walivyokuwa akina Jella Mtagwa, Peter Tino, Juma Pondamali na Mohamed Salim. Maumbo ya aina ile ni nadra kuyaona uwanjani hivi sasa,"alisema.
Mwanasoka huyo mkongwe alisema ujio wa Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil ulisaidia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha soka cha Taifa Stars, ambayo tangu wakati huo, wachezaji wake wamekuwa hawahofii kupambana na timu kama Zambia, Senegal, Morocco, Cameroon na Ivory Coast.
Alisema miaka michache ya nyuma, ilikuwa kitu adimu kwa Taifa Stars kuifunga timu kama Morocco kwa idadi kubwa ya mabao, lakini hilo kwa sasa linawezekana na kwamba kikosi cha timu bora hakiwezi kujengwa kwa siku moja.
"Iwapo Maximo angekuwepo kwa miaka mingi zaidi, hivi sasa tungekuwa mbali sana kisoka kwa sababu alikuwa kocha muhamasishaji,"alisema Razak.
Hata hivyo, mkongwe huyo alieleza pia kuridhishwa kwake na uwezo wa kocha wa sasa wa timu hiyo, Kim Poulsen kutoka Denmark, ambaye amemwelezea kuwa amesaidia kuendeleza kiwango cha timu hiyo kutoka pale alipoishia Maximo.
Kwa mujibu wa Razak, Ivory Coast ilifanikiwa kuifunga Taifa Stars katika michuano ya awali ya Kombe la Dunia kwa sababu ya ujanja na mbinu za kisoka za wachezaji wake. Alisema hata mabao ya Ivory Coast katika mechi hiyo yalikuwa ya kiujanja zaidi kuliko mbinu za kisoka kama ilivyokuwa kwa mabao ya Taifa Stars.
Razak ametoa mwito kwa klabu za soka nchini kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika kukuza na kuendeleza soka ya vijana. Alisema wapo vijana wengi nchini wenye vipaji vya kucheza soka, lakini wanakosa watu wa kuwafuatilia na kuwaendeleza.
Alisema mchezo wa soka hauna mwenyewe duniani na kwamba, timu inayowekeza kwa vijana, inajitengenezea mazingira mazuri ya kutamba miaka ijayo kama zinavyofanya Hispania na Ujerumani.
"Tunapaswa kuwatengeneza vijana wengi zaidi na kuwauza nje ya nchi. Angalia jinsi Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka ya kulipwa DRC walivyoleta mabadiliko makubwa kwa Taifa Stars. Tukiwa na akina Samatta watano, tutakuwa mbali sana kisoka,"alisema.
Aliupongeza uamuzi wa TFF kuzitaka klabu zote za ligi kuu kuwa na timu za vijana wa chini ya miaka 20 na pia kuwepo kwa mashindano ya Copa Coca Cola na Kombe la Uhai, ambayo alisema yamesaidia kuongeza ari ya vijana kushiriki katika mchezo huo.
Razak pia alieleza kufurahishwa kwake kutokana na kampuni nyingi kujitokeza kudhamini mchezo wa soka. Hata hivyo, alisema udhamini huo unapaswa kulenga zaidi timu za vijana kuliko kuwa wa kibiashara zaidi.
Mkongwe huyo alieleza kusikitishwa kwake na vurugu za uongozi zinazotokea mara kwa mara katika vyama vya soka vya mikoa na katika ngazi za klabu. Alisema vurugu hizo zinatokana na kuwepo kwa utitiri wa wafanyabiashara wanaojitosa kwenye uongozi wa mchezo huo kwa lengo la kujineemesha.

No comments:

Post a Comment