KIPA namba moja wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars , Juma Kaseja amewatoa hofu mashabiki wake kwa kuwaambia, hawezi kukosa timu ya kuchezea msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Kaseja alisema atatangaza jina la timu atakayojiunga nayo msimu ujao baada ya pambano la michuano ya Kombe la CHAN kati ya Taifa Stars na Uganda.
Taifa Stars inatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa kumenyana na Uganda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana kati ya Julai 25 na 26 mwaka huu mjini Kampala.
Kaseja alisema kwa sasa ameelekeza nguvu na akili zake katika pambano hilo ili kuhakikisha anaisaidia Taifa Stars kupata ushindi na kujisafishia njia ya kufuzu kucheza fainali za michuano hiyo.
Kipa huyo wa zamani wa Simba alisema, anamshukuru Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kwa kumuamini na kumwita tena kwenye kikosi chake na kuongeza kuwa, jukumu lake ni kudhihirisha kwamba bado yupo juu kisoka.
"Ninachoweza kuwaambia mashabiki wangu ni kwamba siwezi kukosa timu ya kuchezea msimu ujao. Lakini kwa sasa siwezi kuitaja kwa sababu akili yangu iko kwenye pambano letu na Uganda. Nitaitaja baada ya mchezo huo,"alisema kipa huyo, ambaye pia aliwahi kuzidakia Moro United na Yanga.
Kaseja amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi ili kuwapa nguvu na kuwaongezea ari wachezaji na kushinda pambano hilo.
Simba ilitangaza kumtema kipa huyo wiki mbili zilizopita baada ya kutokea mvutano miongoni mwa viongozi wa klabu hiyo, ambapo baadhi walitaka aongezwe mkataba mpya na wengine wakitaka aachwe.
Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, huenda kipa huyo akajiunga na klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro au Coastal Union ya Tanga, japokuwa viongozi wa klabu hizo mbili wamekanusha kuwepo kwa mipango hiyo.
No comments:
Post a Comment