KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, July 27, 2013

TAIFA STARS YATOLEWA KOMBE LA CHAN




MATUMAINI ya timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN) kwa wachezaji wa ndani leo yameota mbawa baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Uganda.

Taifa Stars imepokea kipigo hicho katika mechi ya marudiano iliyochezwa mjini Kampala, Uganda na kuifanya itolewe kwa jumla ya mabao 4-1, kufuatia kuchapwa bao 1-0 katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Dar es Salaam.

Mshambuliaji Frank Kalanda ndiye aliyeibeba Uganda baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Frank aliifungia Uganda bao la kwanza dakika ya 10 baada ya kutokea kizaazaa kwenye lango la Taifa Stars kutokana na mabeki wake kujichanganya.

Taifa Stars ilisawazisha dakika ya 14 kwa bao lililofungwa na Amri Kiemba, aliyeunganisha wavuni krosi maridhawa kutoka pembeni ya uwanja iliyopigwa na Mrisho Ngasa.

Bao la pili la Uganda lilifungwa kwa njia ya penalti na Brian Majweda dakika ya 48 baada ya beki David Luhende kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.

Kosa lililofanywa na kiungo Salum Abubakar dakika ya 62 kutaka kuwapiga chenga mabeki wawili wa Uganda, liliigharimu Taifa Stars baada ya kiungo huyo kupokonywa na mpira na Hassan Waswa, akamgongea Majwega, naye akamsogezea Kalanda aliyefunga bao la tatu.

No comments:

Post a Comment