KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 17, 2013

BABA WA KIEMBA AILIPUA SIMBA



BABA wa mshambuliaji nyota wa klabu ya Simba, Amri Kiemba ameutaka uongozi wa klabu hiyo kumuuza mtoto wake kwa bei ya chini kwa klabu za nje zinazomuhitaji.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, baba huyo mdogo wa Kiemba, aliyejitambulisha kwa jina la Tano Ramadhani alisema, kitendo wanachokifanya Simba kutaka kumuuza mchezaji huyo kwa bei ya juu si halali.

Ramadhani alisema kwa vile mtoto wake amepata bahati ya kuitwa na Raja Casablanca ya Morocco kwenda kucheza soka ya kulipwa, aachwe aende akatafute maisha mapya.

"Viongozi wa Simba wanataka dau kubwa kutokana na kumfanya mchezaji huyo aonekane kama vile ana umri mdogo wakati umri halisi wa Kiemba ni miaka 29," alisema.

Ramadhani alisema viongozi wa Raja Casablanca wameshafika nchini mara kadhaa kwa ajili ya mazungumzo na uongozi wa Simba, lakini wamekuwa wakikwamishwa bila ya sababu za msingi.

Baba huyo alisema kinachotokea hivi sasa ni kama vile viongozi wa Simba wameamua kumuwekea ngumu Kiemba kuondoka baada ya kumsainisha mkataba mpya wa miaka miwili na kumlipa sh. milioni 35.

Amewataka viongozi wa Simba kuacha kuweka mbele maslahi yao binafsi, badala yake watazame mustakabali wa maisha ya mtoto wake, ambaye bado anataka kujiendeleza zaidi kisoka.

"Hata kama Simba wamempa Kiemba shilingi milioni 35, si watazirejesha kutokana na malipo
watakayopewa na Raja Casablanca? Wamuache aende Morocco kutafuta maisha mapya kwa sababu mafanikio yake pia ni ya taifa,"alisisitiza.

Ramadhani alisema yeye kama mzazi, anasikitishwa na uamuzi huo wa Simba kwa vile kiwango cha soka nchini bado kipo chini na Tanzania inahitaji kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka ya kulipwa nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment