'
Wednesday, July 24, 2013
OWINO AOTA MBAWA SIMBA
JUHUDI za viongozi wa klabu ya Simba kutaka kumrejesha beki wa zamani wa timu hiyo, Joseph Owino kutoka Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA), zimegonga mwamba baada ya kukosekana pesa za kumlipa.
Mbali ya kukosekana kwa pesa anazotaka mchezaji huyo, uongozi wa URA umegoma kumuuza Owino kwa Simba kwa vile amepata ofa nzuri ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Qatar, Vietnam na China.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wameshafanya mazungumzo na Owino na kukubaliana naye mambo kadhaa, lakini dau analotaka ni kubwa.
Hata hivyo, Hanspope hakuwa tayari kutaja dau hilo, lakini alisisitiza kuwa bado wanaendelea na juhudi za kutafuta pesa ili waweze kukamilisha usajili wa mchezaji huyo.
Owino aliichezea Simba msimu wa 2009/2010 akiwa na Emmanuel Okwi na Hilaly Echessa kutoka Kenya na kuiletea mafanikio makubwa, lakini aliachwa msimu uliofuata baada ya kuumia goti.
Baada ya kuumia, beki huyo mahiri alipelekwa India kupatiwa matibabu na aliporea nchini alijiunga na Azam FC, lakini alishindwa kuichezea kutokana na kukosa namba na kuamua kurejea Uganda.
Owino alionyesha umahiri mkubwa katika mechi mbili za kirafiki za kimataifa, ambazo URA ilicheza dhidi ya Simba na Yanga. Katika mechi hizo zilizochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, URA iliichapa Simba mabao 2-1 kabla ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Yanga.
"Kimsingi tumeshazungumza na Owino na ameikubali ofa tuliyompa ili aweze kurudi tena Simba, lakini bado kuna masuala yanayohusu pesa, ambayo hatujayakamilisha,"alisema Hanspope.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili ya Simba alisema, kutokana na benchi la ufundi kuvutiwa na kiwango cha beki huyo, watafanya kila wanaloweza kuhakikisha anarejea Msimbazi na kucheza katika ligi kuu msimu ujao.
Wakati Simba ikiwa katika mikakati hiyo, Meneja wa URA, Sam Okabo amesema hawawezi kumruhusu Owino arejee Simba kwa sababu ampata ofa nzuri Marekani na Asia.
Okabo alisema jana kuwa, si rahisi kwa Owino kurejea Simba kama viongozi wa klabu hiyo wanavyotaka kwa vile mchezaji huyo ni lulu kwa sasa na anawindwa na klabu nyingi.
Kwa sasa, Simba imesaliwa na wachezaji wawili wa kigeni, Abel Dhaira na Hamis Tambwe baada ya uongozi kuvunja mkataba wa Mussa Mudde na pia kusitisha mpango wa kumsajili Robert Ssenkoom kutokana na benchi la ufundi kutoridhishwa na kiwango chake.
Katika hatua nyingine, Hanspope amesema mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Hamis Tambwe kutoka Burundi anatarajiwa kuwasili nchini Jumanne na kujiunga na timu hiyo kwenye kambi yake iliyopo Mbamba Beach, Kigamboni, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment