KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 17, 2013

UNAMKUMBUKA MOHAMED SALIM?




UNAPOTAJA jina la Mohamed Salim, bila shaka unawakumbusha mbali mashabiki wa soka nchini, hasa waliowahi kumshuhudia mwanasoka huyo alipokuwa akisakata kabumbu miaka ya 1970 hadi 1980.

Ni mchezaji aliyekuwa na kipaji cha aina yake katika kucheza soka, akiwa na mwili uliojengeka vyema na hivyo kuwapa usumbufu mkubwa mabeki wa timu pinzani katika kumkaba.

Salim (52) alikuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani. Alipoanza kucheza soka, alikuwa akicheza nafasi ya beki wa pembeni, baadaye akacheza nafasi ya beki wa kati, kiungo mkabaji na mwishowe akahamia nafasi ya ushambuliaji, ambayo alidumu nayo hadi alipostaafu soka.

Mshambuliaji huyu ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Coastal Union na timu ya mkoa wa Tanga kung'ara na kutamba kisoka nchini miaka ya 1970 kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao.

Salim pia ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza 1980 zilipofanyika nchini Nigeria. Katika fainali hizo, Taifa Stars ilifungwa na Nigeria na Misri na kutoka sare na Ivory Coast.

Wachezaji wengine waliokuwa wakiunda kikosi hicho wakati huo ni Juma Pondamali, Leopard Tasso, Mohammed Kajole, Ahmed Amasha, Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein, Peter Tino na Thuweni Ally. Kikosi hicho kilikuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama.

Akizungumza na Burudani mjini Tanga hivi karibuni, Salim alisema alianza kucheza soka tangu akiwa mdogo kabla ya kujiunga na timu ya kiwanda cha CIC (sasa Afritex Limited).

Alilazimika kuihama timu hiyo 1970 na kujiunga na Coastal Union baada ya viongozi wa CIC kumfuma akiichezea timu hiyo katika mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi ya Zanzibar. Wakati huo ilikuwa hairuhusiwi mchezaji wa timu ya kampuni kuchezea timu ya mtaani.

Kabla ya kuhama CIC, Salim alisema viongozi wa timu hiyo waliamua kumpa adhabu kwa kumuhamishia katika kitengo, ambacho asingeweza kupata nafasi ya kucheza soka. Aliamua kuwasilisha malalamiko kwa viongozi wa Coastal Union, ambao walimtafutia kazi katika Kiwanda cha Mbolea cha Tanga.

Akiwa kwenye kiwanda hicho, Salim alisema aliweza kupata nafasi ya kuichezea Coastal Union muda wote bila kupata kikwazo chochote. Wakati huo, Coastal Union ilikuwa chini ya kocha marehemu Rashid Moyo

Salim alisema sababu kubwa iliyomfanya ahamie kwenye nafasi ya ushambuliaji ni maajabu aliyoyaonyesha katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Mchakamchaka 1973. Katika mechi hiyo, alianza kucheza nafasi ya beki wa pembeni kulia kabla ya kubadili namba kipindi cha pili na kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati.

"Mechi ilikuwa ngumu na kali. Tulikwenda mapumziko tukiwa hatujafungana. Kipindi cha pili nilimuomba kocha anihamishie nafasi ya ushambuliaji na nikafanikiwa kuifungia Coastal Union mabao matano, yote kwa kichwa. Kuanzia wakati huo, kocha akawa ananichezesha nafasi ya ushambuliaji,"alisema.

Salim alianza kuichezea Taifa Stars 1975 katika michuano ya Kombe la Chalenji ilipofanyika visiwani Zanzibar. Anakiri kwamba, kuteuliwa kwake kwenye kikosi hicho, kilichokuwa chini ya marehemu Mansour Magram, kulimsaidia kukuza kiwango chake kisoka kutokana na kukutana na wachezaji mbalimbali.

Mechi pekee anayoikumbuka alipokuwa akiichezea Taifa Stars ni dhidi ya Nigeria, iliyochezwa 1981. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Lagos, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na ziliporudiana mjini Dar es Salaam, Taifa Stars ilichapwa mabao
2-0.

"Ni mechi iliyojaa ushindani mkali. Nakumbuka baada ya mechi ya marudiano, tulilipwa posho ya shilingi alfu saba kila mchezaji," alisema Salim, ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara katika mji wa Abudhabi nchini Oman.

Siku chache baada ya mechi hiyo, Salim aliondoka nchini kwenda Abudhabi kucheza soka ya kulipwa, akiwa amepata baraka zote kutoka kwa Chama cha Soka nchini (FAT) na serikali. Alikuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kwenda kucheza soka ya kulipwa Arabuni kwa kufuata taratibu zote za kisheria.

Akiwa Abudhabi, Salim alijiunga na klabu ya Al Wahida, ambayo aliichezea kwa miaka 16 hadi 1996 alipoamua kustaafu soka kwa hiari yake kutokana na kupatwa na maumivu ya mguu.

Akiwa katika klabu hiyo, Salim aliwahi kuzawadiwa kiatu cha dhahabu kwa kuibuka mfungaji bora wa ligi 1985 baada ya kufunga mabao 20. Pia aliwahi kuzawadiwa gari jipya aina ya Benz kwa kushinda tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka.

"Nililazimika kustaafu soka kutokana na kusumbuliwa sana na maumivu ya mguu. Nilipofanyiwa uchunguzi hospitali, ikabainika kwamba, mishipa yangu ya damu ya mguu wa kushoto ilikuwa ikiziba,"alisema Salim.

Baada ya kustafu soka, uongozi wa Al Wahida uliamua kumteua Salim kuwa kocha msaidizi katika kikosi cha pili cha timu hiyo na baadaye kupelekwa kusomea fani hiyo barani Ulaya. Baada kumaliza masomo, aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana.

Salim alidumu kwenye kazi hiyo kwa miaka kadhaa kabla ya kuamua kuachana kabisa na soka na kujikita zaidi katika masuala yake binafsi, zikiwemo biashara mbalimbali.

Mwanasoka huyo mwenye uraia wa Oman na ambaye amekuwa akifika Tanga mara kwa mara kwa ajili ya kusalimia ndugu na jamaa alisema, tatizo kubwa linalomwamisha maendeleo ya soka nchini ni wachezaji wa sasa kutocheza kwa ari na kujituma kama ilivyokuwa enzi zao.

Alilitaja tatizo lingine linalokwamisha maendeleo ya mchezo huo kuwa ni uchezeshaji mbovu wa waamuzi, kukosa umakini katika kutekeleza majukumu yao na hivyo kuchangia kuwafanya wachezaji wawe wazembe.

"Kama kweli Tanzania imedhamiria kupiga hatua kimaendeleo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa kuongeza umakini katika utendaji wake wa kazi, ikiwa ni pamoja na kuyafanyiakazi mapungufu yaliyopo sasa,"alisema.

Salim alisema ni vyema shirikisho hilo liandae utaratibu wa kuwashirikisha wadau wa mchezo huo katika kujadili na kuamua masuala mbalimbali muhimu kuhusu mchezo huo badala ya kuwatumia watu, ambao hawana ufahamu wa soka.

Alisema mapenzi waliyonayo baadhi ya viongozi wa shirikisho hilo kwa klabu kubwa na kongwe nchini, yamechangia kudumaza maendeleo ya mchezo huo kwa sababu baadhi ya maamuzi yamekuwa yakitolewa kwa upendeleo.

Salim ametoa mwito kwa wachezaji chipukizi wenye vipaji kufanya jitihada binafsi za kutafuta nafasi za kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi ili waweze kuinua maisha yao badala ya kuridhika na soka ya Bongo.

"Nawashauri wachezaji wetu wasibweteke na kuridhika na mafanikio madogo wanayoyapata hapa nchini. Waongeze bidii zaidi na ikiwezekana wapiganie nafasi ya kwenda kucheza nje ili kuongeza ujuzi na mapato yao,"alisema mkongwe huyo.

Mwanasoka huyo pia amewataka wachezaji wa Tanzania kuzingatia maelekezo ya makocha wao na kujipangia muda wa ziada wa kufanya mazoezi binafsi kwa lengo la kujiweka fiti zaidi kiafya.

"Kuna baadhi ya wachezaji huwa wanafanya vitu tofauti uwanjani na vile wanavyoelekezwa na walimu wao. Hili ni tatizo kubwa lililopo kwa wanasoka wa Tanzania. Wanapaswa kubadilika kwa kufanya kile wanachoelekezwa, sio kufanya wanavyotaka wao,"alisema.

Salim alisema mchezo wa soka kwa sasa umekuwa ukitoa ajira kubwa kwa vijana sehemu mbalimbali duniani, hivyo vijana wa Tanzania wanapaswa kuichangamkia ili waweze kunufaika kimaisha.

"Binafsi naipongeza sana serikali kwa kudhamiria kwa dhati kukuza kiwango cha soka nchini, kuajiri makocha wa kigeni na kuboresha miundombinu. Wanasoka wetu nao wanapaswa kuunga mkono jitihada hizi za serikali kwa kujituma zaidi uwanjani,"alisema.

No comments:

Post a Comment