KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 24, 2013

SHARP STRIKERS FOUNDATION YAPANIA MAKUBWA KISOKA



SOKA ya vijana ndio moyo wa mpira wa miguu nchini. Kwa maana hiyo, kama uwekezaji kwa vijana utafanyika kwa umakini na juhudi kubwa, taifa litapiga hatua kubwa kisoka.
Hakuna nchi iliyofanikiwa duniani katika mpira wa miguu au mchezo wowote bila kuwekeza kwa vijana, ambao ndio nguzo kubwa katika mafanikio.
Kwa kutambua umuhimu huo wa kuwekeza kwa vijana, Sharp Strikers Foundation imejikita katika kuwaendeleza vijana, ambao watakuja kuwa tegemeo katika mchezo wa soka nchini.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Salim Mshamu anasema, Sharp Strikers Foundation inajumuisha mafunzo ya mpira wa miguu kwa watoto wa chini ya miaka 17.
Taasisi hiyo ilianzishwa 2011 kwa kuwafanyia usaili watoto kutoka shule mbalimbali za wilaya ya Korogwe.
“Academy hii ipo katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga na mpaka sasa ina jumla ya watoto 27,”ameeleza Mshamu.
Anasema kuwa ili mtoto aendelee kuwa katika ‘Academy’ hiyo, anatakiwa kufanya vizuri katika masomo yake na kama atafanya vibaya , atasimamishwa na uongozi mpaka pale atakapofanikiwa kujituma katika masomo yake shuleni.
Anaeleza kuwa, wanazingatia masomo kwa kutambua kwamba kwa sasa lazima mchezaji awe wa kisasa kwa kuwa na elimu itakayomwezehaa kufanya mambo kwa umakini mkubwa.
“Kama anafanikiwa kufanya vizuri katika masomo yake, atarudishwa na kuendelea na mafunzo,”ameeleza.
Mshamu anaeleza kuwa, tangu walipoanzisha ‘academy’ hiyo, wameshacheza mechi 25, wameshinda 18, wamefungwa tatu na kutoka sare mechi nne.
“Mechi kubwa tuliyocheza ilikuwa dhidi timu ya Azam ya vijana wa chini ya miaka 17. Mechi ya awali tuliweza kuwafunga mabao 4-0 na katika mechi ya marudiano walitufunga mabao 3-1,”amesema.
Kwa mujibu wa Mshamu, mechi hizo zilichezwa wiki iliyopita katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi. Alisema timu hiyo ilikuwa imefikia katika hoteli ya Serengeti Golden Paradise
Resort, iliyopo Mbande, Mbagala, Dar es Salaam.
Mshamu anasema waliamua kufikia katika hoteli hiyo kutokana na kuwa katika mazingira mazuri kwa utulivu na hivyo kuwapa fursa nzuri vijana wao kuzingatia mafunzo.

No comments:

Post a Comment