KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, July 18, 2013

HUMUD AISHUKIA AZAM



LICHA ya kiungo Abdulhalim Humud  ‘Gaucho’  wa Azam kufuzu majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Jomo Cosmos ya Afrika Kusini, ameshindwa kwenda huko kutokana na kufanyiwa kitu mbaya na Azam.

Humud alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, viongozi wa Azam wamekuwa wakimkwamisha kwenda Afrika Kusini kujiunga na Jomo Cosmos na anashindwa kuelewa ni kwa nini.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba alisema, viongozi wa Azam walitakiwa kufanya mazungumzo na wenzao wa Jomo Cosmos kwa ajili ya uhamisho wake, lakini hadi sasa wameshindwa kufikia makubaliano kuhusu malipo ya ada ya uhamisho.

"Ni kama vile naelea katikati ya bahari, sielewi la kufanya,"alisema kiungo huyo, ambaye jina lake limeachwa katika usajili wa timu hiyo msimu ujao.

Humud alikwenda Afrika Kusini, Aprili mwaka huu na kufanya majaribio hayo Jomo Cosmos kwa wiki mbili na kufaulu. Baada ya majaribio hayo, viongozi wa Jomo Cosmos walimruhusu arudi nyumbani ili waweze kuwasiliana na Azam.

"Namshukuru Mungu kwamba nimeshayafanya ya kwangu na kufanikiwa, sasa nashindwa kuelewa kwa nini viongozi wa Azam wameamua kunikwamisha wakati walitakiwa kujua lini napaswa kwenda Afrika Kusini,"alisema kiungo huyo.

Humud alisema anayo barua aliyopewa na Azam, inayoeleza kwamba yeye ni mchezaji halali wa Jomo Cosmos ndiyo sababu waliamua kumwacha kwenye usajili wa msimu ujao wa ligi.

Kiungo huyo alisema kila anapowafuata viongozi wa Azam na kuwataka wamweleze hatma yake, wamekuwa wakimpiga chenga na hivyo kumweka kwenye wakati mgumu.

Alisema hata nauli ya kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio hayo, alijigharamia mwenyewe wakati alipaswa kulipiwa fedha hizo na Azam. Alisema alitumia dola 800 za Marekani kwa ajili ya safari ya kwenda na kurudi.

"Kila mmoja anasema lake. Hali hii inanipa hasira, napatwa na uchungu. Wanatupigia kelele tunashindwa kwenda nje, kumbe kikwazo ni wao wenyewe,"alisema mchezaji huyo.

Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrisa hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwa vile kila alipokuwa akipigiwa simu, hakupokea wakati msemaji wa klabu hiyo, Jaffer Iddi simu yake ilikuwa haipatikani.

No comments:

Post a Comment