'
Thursday, July 18, 2013
TFF YAFUMUA KAMATI ZAKE
JAJI Steven Ihema na wakili mwandamizi, Bi. Jesse Mguto wataongoza kamati muhimu za za maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoundwa baada ya kufanya mabadiliko kwenye katiba ya Shirikisho hilo mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa TFF Leodegar C. Tenga alitangaza jana.
Shirikisho hilo pia limemteua Jaji Bernard Luanda kuongoza Kamati ya Rufaa za Uchaguzi wakati Profesa Mgongo Fimbo ataendelea kuongoza Kamati ya Rufaa za Nidhamu na Kamanda Mstaafu, Alfred Tibaigana akiendelea kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu.
Rais Tenga alisema hayo wakati alipoongea na waandishi wa habari jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, ambacho kikatiba kina jukumu la kuunda Kamati Ndogo za TFF na vyombo vya maamuzi.
“Tulitaka tuwe na watu solid (imara) na makini ambao watatuhakikishia tunakwenda vyema,” alisema Tenga akizungumzia uteuzi huo ambao unahitimisha mchakato wa mageuzi kwenye Shirikisho baada ya Uchaguzi Mkuu wa TFF uliopangwa kufanyika mwezi Februari kusimamishwa kutokana na baadhi ya wagombea kupinga kuenguliwa na baadaye kwenda FIFA.
Katika kumaliza tatizo hilo, FIFA ilituma ujumbe wake kusikiliza walalamikaji na watu wengine na baadaye kuagiza kuundwa kwa Kamati za Maadili na kufanyika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa TFF kwa ajili ya kuingiza vyombo hivyo kwenye katiba kabla ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa TFF.
“Tumezingatia pia maoni ya wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao walitaka kamati ziwe na majaji... lakini si rahisi kupata seating judges (majaji walio kazini) ndio maana tunawashukuru wale waliotuambia kuwa wako tayari kutusaidia.
“Tumetafuta majaji na mawakili waandamizi ambao tunaamini watatuhakikishia haki inatendeka na inaonekana inatendeka,” alisema Tenga na kuongeza kuwa pia walizingatia maombi ya wajumbe wengine watatu ambao walitaka kupumzika, akiwataja kuwa ni Deo Lyatto, Sylvester Faya na Idd Mtiginjollah.
Alisema kutokana na mfumo huo mpya, mambo yote yanayohusu masuala ya ndani ya uwanja sasa yatashughulikiwa na Kamati ya Nidhamu, wakati yale ya nje ya uwanja, ambayo yanawahusu viongozi na wanafamilia ya mpira wa miguu kwa ujumla, yatashughulikiwa na Kamati za Maadili.
Tenga alisema mabadiliko hayo pia yamegusa kamati nyingine mbili, yaani Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Uchaguzi ambayo sasa itaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Hamidu Mbwezeleni
Jaji Ihema ataongoza Kamati ya Rufaa za Maadili akisaidiwa na mwanasheria mwingine mwandamizi, Victoria Makani, huku Bi. Mguto, ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza vyombo vya vya maamuzi ataongoza Kamati ya Maadili akisaidiwa na makamu wake Francis Kabwe, ambaye Msajili wa Mahakama Kuu.
Katika uteuzi huo, baadhi ya wajumbe wamehamishwa kutoka kamati moja hadi nyingine. Mhe. Murtaza Mangungu, ambaye awali alikuwa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi, sasa ataingia kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili; Kamanda Mohamed Mpinga na Prof Madundo Mtambo wamehamishwa kutoka Kamati ya Rufaa za Uchaguzi kwenda Kamati ya Maadili.
Wajumbe wapya kwenye Kamati hizo ni pamoja na kocha wa zamani wa Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Mshindo Msolla na Kamanda Mstaafu Jamal Rwambow wanaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; mwanasheria maarufu Evodi Mmanda anaingia kwenye Kamati ya Maadili; mwanasheria mwandamizi Mustapha Kambona ambaye anaingia kwenye Kamati ya Nidhamu; Mhe. Mohamed Misanga ambaye anaingia kwenye Kamati ya Maadili na Kanali Iddi Kipingu, ambaye anasifika kwa kuendesha soka la vijana, anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za Nidhamu.
Pia Mwanasheria Anne Steven Marealle anakuwa mjumbe kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi; Yohane Masale (Rufaa za Uchaguzi), Allen Kasamala (Rufaa za Uchaguzi); Francis Kiwanga ambaye pia aningia kwenye Kamati ya Rufaa za Uchaguzi na mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau ambaye anaingia kwenye Kamati ya Rufaa za Maadili.
Kamati ya Utendaji pia imefanya mabadiliko kwenye Kamati ya Waamuzi ambako mwenyekiti Said Nassoro na katibu Charles Ndagala wa Chama cha Waamuzi wanaingia kwenye kamati hiyo kushika nafasi ya Joan Minja na Riziki Majala.
Wajumbe wa Kamati hizo ni kama ifuatavyo:
Kamati ya Rufaa za Maadili ni Jaji Steven Ihema (mwenyekiti), Victoria Makani (m/mwenyekiti), Mhe. Mohamed Misanga, Henry Tandau na Mhe. Murtaza Mangungu.
Kamati ya Maadili: Bi Jesse Mguto (mwenyekiti), Francis Kabwe (m/mwenyekiti), ACP Mohamed Mpinga, Prof. Madundo Mtambo, na Evod mmanda.
Kamati ya Rufaa za Nidhamu: Prof. Mgongo Fimbo, Ong’wanuhama Kibuta (m/mwenyekiti), Kanali Mstaafu Idd Kipingu, Dk. Mshindo Msolla, ACP Jamal Rwambow.
Kamati ya Nidhamu: Kamanda Mstaafu Alfred Tibaigana (mwenyekiti), Mustafa Kambona (m/mwenyekiti), Azzan Zungu, Yussu Nzowa na Mohamed Msomali.
Kamati ya Rufaa za Uchaguzi: Jaji Bernard Luanda (mwenyekiti), Francis Kiwanga (m/mwenyekiti), A. Steven Semu, Yohane Masalla na Allen Kasamala.
Kamati ya Uchaguzi: Hamidu Mbwezeleni (mwenyekiti), Moses Kaluwa (m/mwenyekiti), Mustafa Siani, Hassan Dyamwale na Kitwana Manara.
Kamati ya Waamuzi: Kapteni Mstaafu Stanley Lugenge (mwenyekiti), Omar Kasinde (m/mwenyekiti), Said Nassoro, Charles Ndagala na Mohamed Nyama.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment