KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, July 26, 2013

TAIFA STARS YATUA UGANDA, MECHI KUCHEZWA KESHO



Taifa Stars imewasili salama hapa Kampala tayari kwa mechi ya marudiano ya mchujo dhidi ya Uganda (The Cranes) kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Tatu za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Stars ambayo iliwasili ikitokea jijini Mwanza ilipokuwa imepiga kambi ya siku kumi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoamua ni timu ipi kati ya hizo mbili itakwenda Afrika Kusini mwakani imefikia hoteli ya Mt. Zion iliyoko eneo la Kisseka katikati ya Jiji la Kampala.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ameridhishwa na kiwango cha hoteli hiyo, kwani ndiyo ambayo timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ilifikia Novemba mwaka jana ilipokuja Kampala kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Stars ambayo ilitiwa chachu na Rais Jakaya Kikwete alipokutana nayo Uwanja wa Ndege wa Mwanza wakati ikiondoka kuja Kampala, na kuitakia kila la kheri itafanya mazoezi yake ya mwisho kesho (Julai 26 mwaka huu) Uwanja wa Mandela kujiandaa kwa mechi ya Jumamosi.

Kocha Kim amesema ingawa mechi hiyo ni ngumu, lakini kikosi chake kimejiandaa kuikabili Uganda kwani wachezaji wako wako vizuri na ari kwa ajili ya mechi iko juu.

Wachezaji wote wako katika hali nzuri, isipokuwa Khamis Mcha aliyekuwa na maumivu ya goti, lakini kwa mujibu wa madaktari wa timu anaendelea vizuri kwani tayari wanampa mazoezi mepesi.

Kikosi cha kamili cha Stars ilichoko hapa kinaundwa na makipa Juma Kaseja, Mwadini Ali na Ali Mustafa. Mabeki ni Aggrey Morris, David Luhende, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Nadir Haroub na Vincent Barnabas.

Viungo ni Amri Kiemba, Athuman Idd, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Khamis Mcha, Mudhathir Yahya, Salum Abubakar na Simon Msuva. Washambuliaji ni John Boko, Juma Luizio na Mrisho Ngasa.

Wakati huo huo, Kocha Kim Poulsen atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari siku ya Jumatatu (Julai 29 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika saa 5 kamili asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

No comments:

Post a Comment