'
Wednesday, July 17, 2013
MNIGERIA AMTIMUA KIIZA
UONGOZI wa klabu ya Yanga umeshindwa kumpa mkataba mpya mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamis Kiiza baada ya mchezaji huyo kushinikiza alipwe sh. milioni 45.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, Kiiza alikuwa anataka alipwe fedha hizo zote ndipo atie saini mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.
Kwa mujibu wa habari hizo, uongozi wa Yanga ulitaka kumpa mchezaji huyo sh. milioni 20 ili aweze kutia saini mkataba huo mpya na kumaliziwa fedha zilizobaki baadaye.
"Jambo hilo limewaudhi viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga na wameamua kuachana naye na kuendelea na mipango ya kumsajili mshambuliaji mpya kutoka Nigeria," kilisema chanzo hicho cha habari.
Mshambuliaji huyo mpya kutoka Nigeria, Ogbu Brendan Chukwudi aliwasili nchini juzi usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya Airways na kupokewa kwa mbwembwe na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.
Chukwudi, ambaye alikuwa akichezea klabu ya Heartland ya Nigeria, alitarajiwa kuanza mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake jana kwa ajili ya kupimwa uwezo wake na Kocha Ernie Brandts kabla ya kupewa mkataba.
"Upo kila uwezekano wa nafasi ya Kiiza kuchukuliwa na Mnigeria kwa sababu Kiiza ameonyesha jeuri na kutaka alipwe fedha nyingi kuliko wachezaji wenzake," kilieleza chanzo hicho cha habari.
Awali, mjumbe wa kamati ya usajili ya Yanga, Musa Katabalo alitumwa kwenda Uganda kwa ajili ya kuzungumza na Kiiza na kufanikiwa kuja naye Dar es Salaam kwa mazungumzo zaidi.
Kiiza, ambaye alikuja nchini na kikosi cha Uganda, kilichocheza mechi ya michuano ya Kombe la CHAN dhidi ya Taifa Stars, alifanya mazungumzo na viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini walishindwa kufikia mwafaka.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Kiiza alisema bado yeye ni mchezaji huru na anaweza kujiunga na klabu yoyote kwa vile mkataba wake na Yanga ulishamalizika.
Kiiza alikiri kufanya mazungumzo na viongozi wa kamati ya usajili ya Yanga na kusisitiza kuwa, walishindwa kufikia mwafaka baada ya viongozi hao kugoma kumlipa sh. milioni 45 kwa mara moja.
Mchezaji huyo hakuwa tayari kuweka wazi iwapo ni kweli aliamua kurejea katika klabu yake ya awali ya Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA) kama baadhi ya vyombo vya habari nchini vilivyoripoti wiki iliyopita.
Wakati huo huo, Yanga leo inatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Three Pillare ya Nigeria katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment