KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 17, 2013

WACHEZAJI SIMBA WATEMBELEA KABURI LA BABA WA TAIFA



WACHEZAJI wa timu ya soka ya Simba juzi walitembelea kaburi la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere lililopo nyumbani kwake kijiji cha Mwitongo kilichopo Butiama mkoani Mara.

Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, mbali na kutembelea kaburi hilo, wachezaji wa timu hiyo pia walipata nafasi ya kuzungumza na familia ya Nyerere.

Kamwaga alisema ziara hiyo nyumbani kwa Baba wa Taifa, ilikuwa ni sehemu ya ziara ya Simba katika mkoa wa Mara, ambako inatarajiwa kucheza mechi kadhaa za kirafiki dhidi ya timu za mkoa huo.

Kwa mujibu wa Kamwaga, Simba ilitarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza jana dhidi ya Kombaini ya mkoa wa Mara kabla ya kuvaana na timu ya Polisi, ambayo ni mabingwa wa mkoa huo.

Ofisa huyo wa Simba alisema kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kurejea Dar es Salaam kesho kwa ajili ya pambano lao la kimataifa la kirafiki dhidi ya URA ya Uganda litakalofanyika keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Katika hatua nyingine, Kamwaga amesema maandalizi ya mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika keshokutwa yanaendelea vizuri.

Kamwaga alisema jana kuwa, mkutano huo utafanyika kwenye bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam na amewataka wanachama wa Simba kujitokeza kwa wingi kuhudhuria.

Alisema wanachama watakaoruhusiwa kuhudhuria mkutano huo ni wale waliolipia kadi zao na kuonya kuwa, wanachama watakaothubutu kufanya fujo, watachukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment