KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 17, 2013

KAPOMBE HUYOOO UHOLANZI


BEKI kiraka wa klabu ya Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars, Shomari Kapombe anaondoka nchini kesho kwenda Uholanzi kwa ajili ya kufanyiwa majaribio ya kucheza soka ya kulipwa.

Kapombe anaondoka nchini baada ya kupata ruhusa kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Kim ameridhia Kapombe kuondoka licha ya timu yake kukabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Uganda.

Taifa Stars imeweka kambi mjini Mwanza kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la CHAN dhidi ya Uganda itakayochezwa kati ya Julai 26 na 28 mjini Kampala.

Katika mechi ya awali iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Taifa Stars ilichapwa bao 1-0 na hivyo kujiweka kwenye mazingira magumu ya kufuzu kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Angetile, Kim ameridhia mchezaji huyo kwenda Uholanzi kwa kuzingatia kuwa, mafanikio yake yatakuwa sifa kubwa kwa Tanzania.

Kapombe anatakiwa kufanya majaribio hayo katika klabu ya FC Twente ya Uholanzi, ambayo inashiriki katika ligi kuu ya nchi hiyo.

Awali, Kapombe alitakiwa kuondoka nchini Juni 28 na baadaye Julai 15 mwaka huu kwenda Uholanzi, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na Taifa Stars kukabiliwa na mechi muhimu dhidi ya Ivory Coast na Algeria.

Mbali na FC Twente, Kapombe pia anatarajiwa kufanya majaribio katika klabu zingine za ligi kuu ya Uholanzi.

No comments:

Post a Comment