BEKI wa zamani wa klabu ya Simba, Amir Maftah amesema bado hajafanya mazungumzo na timu yoyote kwa ajili ya kuichezea katika msimu ujao wa ligi kuu.
Akizungumza na Burudani kwa njia ya simu juzi, Maftah alisema kwa sasa anakabiliwa na majukumu mengi ya kifamilia hivyo hawezi kuzungumzia masuala ya usajili.
Hata hivyo, Maftah alisema anatarajia kujua wapi pa kwenda baada ya siku chache zijazo. Ligi kuu ya Bara imepangwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.
Maftah alisema tangu alipotofautiana na uongozi wa Simba na kusimamishwa kuichezea timu hiyo, amekuwa akifanya mazoezi kwa kujitegemea kwa lengo la kujiweka fiti.
"Nilikuwa nyumbani Mwanza kushughulikia matatizo ya kifamilia, nimerudi Dar es Salaam siku chache zilizopita. Natarajia kuanza mazungumzo na klabu mbalimbali siku chache zijazo,"alisema.
Beki huyo wa zamani wa Taifa Stars alisema tayari klabu kadhaa za ligi kuu zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili, lakini bado hajaamua wapi pa kwenda.
Maftah, ambaye amewahi kung'ara katika klabu za Mtibwa Sugar, Yanga na Simba, alisimamishwa pamoja na wachezaji wenzake watano kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Kauli ya beki huyo imekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti wiki iliyopita kuwa, anatarajia kujiunga na Coastal Union ya Tanga kwa ajili ya msimu ujao.
Hata hivyo, mmoja wa wakurugenzi wa Coastal Union, Bin Slum alikanusha taarifa hizo na kusema hawana mpango wa kusajili mchezaji mwingine kutoka Simba. Tayari Coastal Union imeshawasajili Haruna Moshi 'Boban' na Juma Nyosso.
No comments:
Post a Comment