Hilal pia ndiye kocha mkuu wa timu hiyo, ambayo imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi daraja tatu na pia kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iliyomalizika wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga baada ya kuishinda Makorola kwa penalti 5-4.
Kazi kubwa ilikuwa ni kumshawishi Hilal kuzungumza naye masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake soka. Ni kwa sababu huwa hapendi kuzungumza na vyombo vya habari. Hapendi kuhojiwa jambo lolote kuhusu maisha yake kisoka.
"Hata nilipokuwa Oman, kila waandishi wa habari walipokuwa wakinifuata, nilikuwa nikiwaambia andikeni mlichokiona uwanjani. Huwa sipendi kabisa kuzungumza na vyombo vya habari,"alisema Hilal nilipokutana naye wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
"Naweza kusema wewe una bahati kwa sababu ulianza kunipigia simu mapema na umefunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Tanga. Nimeona kukukatalia, lisingekuwa jambo la kistaarabu," aliongeza nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania.
Jina la Hilal si geni kwa mashabiki wa soka nchini, hasa wa miaka ya 1980. Alikuwa mchezaji mwenye kipaji cha aina yake, akiwa na uwezo mkubwa wa kuwatoka mabeki wa timu pinzani anavyotaka na pia kufunga mabao.
Uwezo huo wa Hilal ndio uliomfanya awindwe kwa udi na uvumba na klabu za Arabuni wakati huo na hatimaye kuondoka nchini kwa siri mwaka 1984 kwa kupitia nchi jirani ya Kenya, akihofia kuzuiwa.
Mpango huo wa kwenda Arabuni pia ulimuhusisha beki nyota wa zamani wa klabu ya Yanga, Ahmed Amasha, ambaye aliondoka nchini wiki moja kabla ya Hilal. Amasha naye aliondoka nchini kwa siri kwa kupitia Kenya, akihofia kuzuiwa na viongozi wa klabu ya Yanga.
Hilal aliondoka nchini miaka miwili baada ya kuichezea Coastal Union ya Tanga kwa mafanikio makubwa msimu wa 1983 na 1984. Pia alikuwa mmoja wa wachezaji wa timu ya Tanzania Bara, iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji 1984 ilipofanyika nchini Uganda.
Katika michuano hiyo, mshambuliaji huyo aliyekuwa na kipaji cha kuzifumania nyavu, ndiye aliyeifungia Tanzania Bara bao la kusawazisha ilipotoka sare na Uganda kwenye uwanja wa Nakivubo. Pia ndiye aliyeifungia bao Tanzania Bara ilipofungwa mabao 2-1 na Zambia.
Nyota ya Hilal kisoka ilianza kung'ara 1982 alipojiunga na Coastal Union akitokea timu ya vijana ya African Sports. Hakuweza kuichezea timu hiyo katika msimu wa kwanza baada ya kufungiwa na Chama cha Soka cha Tanga kwa tuhuma za kusajiliwa na timu mbili, ikiwemo Mchakamchaka.
Aliichezea timu hiyo msimu wa 1983 na 1984 akiwa na baadhi ya wanasoka nyota wa zamani kama vile Saidi Jacky, Bakari Jacky, Hemed Morocco, Duglas Muhani, Abdalla Shamimu, Salim Omar, Titus Bandawe na Elisha John.
Kung'ara kwake katika michuano ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara wakati huo, ndiko kulikomfanya aitwe kwenye kikosi cha Tanzania Bara na hatimaye kuichezea katika michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika Uganda.
"Naikumbuka sana mechi yetu dhidi ya Uganda kwa sababu ilikuwa ya kwanza kwangu kubwa na ilikuwa ngumu. Uwanja ulikuwa umefurika mashabiki ile mbaya. Baada ya waganda kutufunga, nilifanikiwa kufunga bao la kusawazisha," alisema Hilal.
Mtanzania aliyekuwa akifahamika kwa jina la Swalehe, aliyekuwa akiishi Oman wakati huo, ndiye aliyemfungulia Hilal milango ya heri ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Arabuni baada ya kumuona na kuvutiwa na kiwango chake kisoka alipokuwa akiichezea Taifa Stars mjini Mwanza.
"Huyu mzee ni Mtanzania aliyekuwa akiishi Oman. Alinifuata siku moja nikiwa na Amasha na kunieleza kwamba habari zangu zote zimeshafika Oman na ningeletewa viza wakati wowote kwa ajili ya kwenda huko," alisema Hilal.
Baada ya kufika Arabuni, Hilal alijiunga na klabu ya Fanja ambayo aliichezea kwa misimu tisa akiwa na baadhi ya wanasoka wenzake nyota kutoka Tanzania, kama vile marehemu Ramadhani Lenny, Twalib Hilal, Amasha, Madaraka Selemani, Zahor Salum na Abdul Wakati Juma.
Akiwa Fanja, Hilal aliweka rekodi ya kutwaa nayo taji la kwanza la ubingwa wa ligi ya Oman 1989 kabla ya kutwaa nayo mataji mengine matatu. Pia aliweka rekodi ya kutwaa nayo Kombe la Mfalme wa Oman mara tatu.
Hilal aliihama Fanja 1993 baada ya kununuliwa na klabu ya Dhofar yenye maskani yake katika mji wa Salala. Aliichezea klabu hiyo kwa miaka tisa na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Oman mara nne na Kombe la Mfalme mara moja.
Katika kikosi cha Dhohar, Hilal alicheza pamoja na Amasha, Gabriel Olanga, Douglas Mutua, Benard Otieno na Vitalis Oduor kutoka Kenya pamoja na Shock Gharib kutoka Misri, ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Wachezaji wengine walikuwa wazawa.
Hilal aliamua kutundika daruga zake ukutani 2002 kwa kile alichokieleza kuwa ni kupumzika baada ya kucheza soka kwa miaka mingi. Lengo lake kubwa lilikuwa kutoa nafasi kwa wanasoka wengine chipukizi kuonyesha uwezo wao.
Mwanasoka huyo alisema alitamani sana kwenda kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya, lakini ilikuwa vigumu kwa mchezaji anayetokea Arabuni kupata nafasi hiyo. Alisema anasikitika kwa kuikosa nafasi hiyo kwa vile ilikuwa ndoto yake kubwa kutokana na kuwa na sifa zote za kucheza soka ya kulipwa Ulaya.
Baada ya kustaafu soka, Hilal aliweza kusafiri katika nchi mbalimbali za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Uholanzi, ambako aliishi kwa miaka kadhaa. Pia amewahi kutembelea Brazil zaidi ya mara tatu.
Hilal alisema anamshukuru Mungu kwamba mchezo wa soka umemwezesha kufanikisha mambo yake mengi, ikiwa ni pamoja na kuwa na maisha mazuri kutokana na kulipwa vizuri na klabu zote mbili alizokuwa akizichezea Arabuni.
"Wakati nilipokuwa nikicheza soka, nilihakikisha nafanyakazi kisawasawa. Sikuwa na mchezo katika kazi yangu. Nilikuwa mfungaji nyota wa mabao. Namshukuru Mungu alinijalia kipaji cha kucheka na nyavu. Hadi leo hii, nina jina kubwa Arabuni,"alisema Hilal.
Aliongeza: "Nilifanya vizuri sana nilipokuwa Fanja. Ilikuwa kila mechi, sikosi kufunga bao. Nikikukosa leo, lazima mechi inayofuata nikufunge."
Hilal alisema hakuweza kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars baada ya kwenda Arabuni kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu wa kufuatilia wachezaji wanaocheza nje ya nchi kama ilivyo sasa. Alisema utaratibu wa zamani wa makocha waliowahi kuifundisha Taifa Stars, ulikuwa ni kufuatilia wachezaji wanaocheza ligi za ndani.
Alisema makocha hao pamoja na viongozi wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) waliwadharau wachezaji waliokwenda Arabuni kwa kudhani kiwango cha soka katika nchi hizo ni duni.
"Lakini kusema ukweli, timu za Arabuni zilikuwa zikifundishwa na makocha wazuri na wenye uwezo mkubwa, kulikuwa na viwanja vizuri vya mazoezi, wachezaji walikuwa wanalipwa vizuri na timu zilikuwa zikiweka kambi katika baadhi ya nchi za Ulaya. Kwa jumla kulikuwa na kila kitu cha kumfanya mchezaji acheze soka kwa uwezo wake wote,"alisema.
Hilal anakiri kwamba, kiwango cha soka nchini miaka ya nyuma kilikuwa juu ikilinganishwa na sasa kwa vile wachezaji walicheza kwa ari kubwa na kujitolea kutokana na kuupenda mchezo huo.
Alisema ari waliyokuwa nayo wachezaji wa zamani ingekuwepo sasa, Tanzania ingekuwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
Hata hivyo, Hilal alisema kiwango cha sasa kisoka kinaridhisha kutokana na kuwepo kwa mwamko kutoka kwa serikali na kampuni mbalimbali, ambazo zimeamua kuwekeza fedha zake ama kujitangaza kibiashara kupitia soka.
"Taifa Stars ya zamani haikuwa na mdhamini, ilikuwa ikisaidiwa na serikali, lakini wachezaji walicheza kwa ari kubwa. Hivi sasa kuna mabadiliko makubwa. Baadhi ya klabu zimekuwa zikiajiri makocha na wachezaji wa kigeni na hivyo kuongeza ushindani,"alisema.
Pamoja na kuwepo kwa ushindani wa klabu kusajili wachezaji wa kigeni, Hilal alisema haridhishwi na viwango vya baadhi yao kwa vile ni vya chini ikilinganishwa na wazawa. Alisema baadhi ya wachezaji wa kigeni wanapewa sifa na vyombo vya habari wakati uwezo wao ni mdogo.
Hilal alisema si rahisi kwa mchezaji kutoka Cameroon, Ghana au Nigeria kuja kucheza soka ya kulipwa Tanzania na kuongeza kuwa, wanaofanya hivyo wanafuata fedha kwa kulazimisha.
"Mimi nimeishi Uholanzi kwa miaka 10 baada ya kustaafu soka. Nimeona jinsi wachezaji wa kigeni wanavyotafutwa. Hakuna mchezaji wa kigeni anayechukuliwa akiwa na umri wa miaka zaidi ya 25,"alisema.
Hilal amelishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa mafunzo ya utawala kwa wanasoka wa zamani ili waweze kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za chini hadi Taifa. Alisema ni aibu kwa vyama vya michezo nchini kuongozwa na watu, ambao hawajahi kucheza soka na kufikia hatua ya kuichezea timu ya taifa ama hawana elimu yoyote kuhusu uongozi wa michezo.
"Uongozi wa soka lazima wapewe wanaojua soka na wafanyabiashara waendelee na biashara zao. Hata ukitazama katika nchi za Ulaya, wanasoka wastaafu ndio wanaopewa uongozi katika klabu na vyama vya michezo,"alisema.
Hilal alisema Tanzania haipaswi kuendelea kuwa na mizengwe iliyopo sasa katika uongozi wa soka na kwamba wachezaji wa zamani wanapaswa kupewa elimu ya uongozi wa mchezo huo ili washike madaraka.
Aliupongeza uongozi wa Coastal Union kwa kuwashirikisha wanasoka wake wa zamani kuunda benchi la ufundi. Alisema utaratibu huo utaisaidia klabu hiyo kupata mafanikio makubwa zaidi kisoka katika miaka michache ijayo.
Hilal pia alimpongeza Rais wa TFF, Leodegar Tenga kwamba ni kiongozi mzuri na aliyeleta mabadiliko makubwa katika shirikisho hilo kwa vile alicheza soka, lakini kelele zinazosikika sasa katika uongozi wake zinatokana na wasaidizi wake kushindwa kumsaidia.
Ameitaka TFF kuendelea kutoa kipaumbele kwa soka ya vijana kwa vile ndiyo msingi mzuri katika kuwaandaa wanasoka wa baadaye. Pia alizipongeza klabu za ligi kuu kwa kuwa na timu za vijana wa chini ya miaka 20.
Hata hivyo, Hilal alisema haitakuwa na maana kwa klabu hizo kuwa na timu vijana, lakini haziwathamini. Alisema timu za vijana zinapaswa kupewa hadhi sawa na za wakubwa ili kuwaongezea ari ya kufanya vizuri zaidi.
"Duniani kote, wachezaji wanaanza kuandaliwa wakiwa vijana. Wachezaji waliopo sasa katika timu ya Taifa ya Hispania walianza kuandaliwa tangu wakiwa wadogo. Ndio sababu unaona mbali na kutwaa ubingwa wa dunia, Hispania imetwaa ubingwa wa Ulaya na wa timu za vijana wa chini ya miaka 21,"alisisitiza mwanasoka huyo.
Hilal ameishauri TFF kuzipigania klabu za ligi kuu ili ziwe na ufadhili badala ya ilivyo sasa, ambapo baadhi ya timu zinashiriki ligi kwa matatizo kutokana na kukosa fedha. Alisema ni aibu kwa timu ya ligi kuu kukosa fedha za kusafiria kutoka kituo kimoja au kingine ama kukosa pesa za chakula na kuwalipa posho wachezaji wake.
"Nimecheza soka Arabuni kwa miaka 18, sijawahi kusikia timu imekwama kusafiri kwenda kituo cha ligi kwa kukosa pesa. Ni lazima tuondokane na uendeshaji soka wa aina hii. Ikiwezekana timu zisafirishwe kwa ndege na kupangiwa kwenye hoteli nzuri,"alisisitiza.
Hilal pia ameitaka TFF kurejesha utaratibu wa klabu mwenyeji katika ligi kuchukua mapato yote ili kuziwezesha kujikwamua kiuchumi. Ikiwezekana, Hilal alisema ni vyema kila klabu ikawa na uwanja wake ili ziweze kunufaika zaidi kimapato.
Hilal alizaliwa 1967 mkoani Tanga. Alisoma shule ya msingi ya Chuma kuanzia 1975 hadi 1981 alipomaliza darasa la saba. Alianza kucheza soka tangu akiwa shule ya msingi na pia alichezea timu ya mtaani ya Bomboka kabla ya kujiunga na timu ya African Sports Kids.
No comments:
Post a Comment