KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, July 24, 2013

NSAJIGWA: KLABU ZIACHE KASUMBA YA KUAJIRI MAKOCHA WA KIGENI


SHADRACK Nsajigwa 'Fuso' ni jina maarufu katika soka ya Tanzania. Ni beki aliyejizolea sifa kemkem kutoka kwa mashabiki wa mchezo huo nchini kutokana na uwezo wake wa kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani na pia kupanda mbele kusaidia mashambulizi. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE, nahodha huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, ambaye amestaafu soka, anaelezea mikakati yake katika kazi yake mpya ya ukocha wa soka.

SWALI: Hongera kwa kuhitimu mafunzo ya ukocha wa soka na pia kuajiriwa na klabu ya Lipuli ya Iringa ukiwa kocha mkuu. Ni kipi kilichokuvutia ukaamua kujitosa kwenye fani hiyo?

JIBU: Mchezo wa soka upo kwenye damu yangu. Nilishajipanga mapema kwamba,baada ya kustaafu soka, niendelee kutoa mchango wangu katika mchezo huo kwa kufundisha timu za madaraja mbalimbali.Ni ndoto niliyokuwa nayo kwa muda mrefu.

Ndio sababu kabla hata sijaamua kustaafu soka, nilianza kuchukua mafunzo ya ukocha wa mchezo huo kuanzia katika ngazi mbalimbali na leo hii naweza kujivuna kwa kufanikisha azma yangu hiyo kwa vile ninacho cheti cha kuniwezesha kupata kazi ya ukocha sehemu yoyote hapa nchini na kwa kuanzia, nimeanza kazi hiyo Lipuli.

Mbinu nyingi za kufundisha soka nimezipata kupitia mafunzo mbalimbali niliyopita, lakini nyingine nimezipata kwa sababu ya utundu kutokana na kufundishwa na makocha tofauti katika timu zote nilizochezea.

SWALI: Pamoja na kuipenda kwako kazi hii ya ukocha, huoni kwamba ni ya lawama, hasa iwapo timu itafanya vibaya ama kushindwa kutimiza malengo yake?

JIBU: Ni kweli kazi ya ukocha ina lawama, cha msingi ni kuwa mvumilivu kwa sababu hakuna kazi ya mteremko. Ni kazi ambayo ninaipenda na ninaujua ugumu wake, hivyo nipo tayari kukabiliana na changamoto zozote nitakazokumbana nazo.
Lengo langu kubwa ni kuinua vipaji vya vijana na kuwaendeleza. Sijaridhika kwa elimu niliyoipata kwa sasa. Nitatafuta wadhamini ili waweze kuniendeleza na kuwa kocha wa ngazi za juu zaidi.

SWALI: Ni kawaida ya mashabiki wa soka nchini kuwatolea lugha chafu makocha timu inapofanya vibaya ama kutolewa kafara na uongozi timu inapofungwa mfululizo. Je, upo tayari kukabiliana na changamoto hizi?

JIBU: Kama nilivyokueleza mwanzo, nipo tayari kwa lolote kwa sababu hii ndiyo kazi niliyoamua kuifanya baada ya kustaafu kucheza soka. Binafsi nimevumilia mengi sana nilipokuwa nikiichezea Yanga, ambayo siwezi kuyataja kwa sababu mimi ni mtu mzima, hivyo nina uwezo wa kuvumilia lolote katika kazi yangu hii mpya.

SWALI: Unazungumziaje kasumba iliyopo sasa ya klabu kubwa na zenye uwezo wa kifedha nchini kupenda kuajiri makocha wa kigeni na kuwadharau makocha wazalendo?

JIBU: Kuajiri kocha wa kigeni sio dhambi kwa sababu wakati mwingine wanasaidia kuongeza ujuzi kwa wachezaji wetu na makocha wazawa. Lakini nadhani wakati umefika kwa viongozi wa klabu kubwa nchini kutoa ajira kwa makocha kwa kuzingatia sifa na uwezo wao badala ya kukimbilia makocha wa kigeni, ambao wamekuwa wakilipwa fedha nyingi, lakini kazi wanayoifanya ni ndogo sana.

Kwa kipindi chote nilichocheza soka, nimekutana na kufundishwa na makocha wengi wa kigeni, hivyo najua uwezo na udhaifu wa baadhi yao. Naweza kusema kwamba, baadhi yao walikuwa wababaishaji. Hivyo ni vyema tuwape nafasi makocha wetu wazawa ya kuonyesha uwezo wao kama zinavyofanya baadhi ya timu za ligi kuu za hapa nchini.

SWALI: Ungependa kutoa mwito gani kwa wanasoka wenzako wa zamani, ambao baada ya kustaafu soka, wamekuwa na maisha magumu na pengine hawana la kufanya?

JIBU: Moja ya sababu zilizonifanya niamue kuchukua mafunzo ya ukocha ni kujiandaa kwa maisha yangu ya baadaye baada ya kuwaona baadhi ya wachezaji waliotutangulia wakihangaika. Na hii ndio sababu iliyonifanya niamue kuendelea na mafunzo ya ngazi za juu zaidi ya ukocha ili niweze kutambulika kama kocha wa kimataifa.

Baadhi ya wakati ninapokutana na wachezaji wenzangu wa zamani, huwa nawashawishi kutafuta kitu cha kufanya baada ya kustaafu soka kwa sababu umaarufu hauwezi kuwasaidia lolote. Tunapaswa kujiandaa kwa maisha yetu ya baadaye.

SWALI: Unadhani umestaafu kucheza soka kwa heshima baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka kadhaa?

JIBU: Mwanamichezo yoyote aliyeipatia sifa klabu na nchi yake, anapaswa kuwa na malengo ikiwa ni pamoja na kustaafu akiwa bado na heshima badala ya kusubiri kudhalilishwa. Nimeamua kustaafu soka nikiwa bado nina uwezo, lakini nimeamua kutoa nafasi kwa vijana chipukizi kuonyesha uwezo wao. Uamuzi nilioufanya unapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wachezaji wengine.

SWALI: Unao ushauri wowote kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu wanasoka wa zamani?

JIBU: Naishauri TFF iwasaidie wanasoka wa zamani kupata mafunzo ya ukocha ili waweze kuendelea kutoa mchango wao katika kuinua mchezo huu. Na ni vyema makocha hawa watumike kufundisha timu za vijana kwa lengo la kuibua vipaji vyao na kuwaendeleza.

SWALI: Unapenda kuwaeleza kitu gani viongozi wetu wa soka hapa nchini?

JIBU: Wanapaswa kuweka mbele zaidi maslahi ya wachezaji badala ya kuweka mbele maslahi yao binafsi. Wakumbuke kuwa, wachezaji ndio wanaovuja jasho uwanjani, hivyo wanapaswa kuthaminiwa kwa kulipwa haki zao zote na kwa wakati pasipo kudhulumiwa.

Napenda pia kuwashauri viongozi wa soka nchini, wawakatie bima wachezaji wao ili wawe na kinga baada ya kuumia, badala ya ilivyo sasa, ambapo wachezaji wengi hawana bima, hivyo wanapoumia uwanjani, hakuna wa kuwatibia na viongozi wamekuwa wakiwatelekeza.

Vilevile nawashauri viongozi wa klabu za ligi kuu na zinginezo, kuwaingiza wachezaji wao kwenye mifuko ya pensheni ili waweze kuchangia na kunufaika na makato yao baada ya kustaafu soka.

No comments:

Post a Comment